Yanga Yatuma Ujumbe Mzito Kwa MC Alger, Yasema “Tunabonda Huku Tunanyonga”

Klabu ya Yanga imetuma ujumbe wa hamasa kuelekea mchezo wake wa kwanza wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya MC Alger ya Algeria, ikitumia kauli mbiu isemayo “Tunabonda Huku Tunanyonga” kuelezea dhamira yake ya kufanya vizuri katika michuano hiyo.

Kupitia bango la mchezo huo lililowekwa katika muonekano wa kijani na njano, Yanga imewaonesha baadhi ya nyota wake wakiwa katika jezi za klabu hiyo, huku ujumbe huo ukionesha dhamira ya Wananchi kuanza kampeni yao ya Afrika kwa nguvu.

Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Jumamosi, Novemba 28, 2026, katika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, kuanzia saa 10:00 jioni kwa saa za Afrika Mashariki.

Yanga inaingia katika mchezo huo ikiwa na jukumu la kuanza vizuri kampeni yake ya Kundi B, ambako imepangwa pamoja na MC Alger, Zamalek ya Misri na Club Africain ya Tunisia.

Katika hatua nyingine, uongozi wa Yanga kupitia Meneja wa Habari na Mawasiliano, Ali Kamwe, umewahamasisha mashabiki kujitokeza kwa wingi visiwani Zanzibar ili kuhakikisha Uwanja wa New Amaan Complex unajaa katika mchezo huo muhimu.

Klabu hiyo pia imetangaza viingilio vya mchezo huo ambapo tiketi za majukwaa ya Saa na Obit ni Shilingi 5,000, Urusi Shilingi 10,000, Wings Shilingi 20,000 na VIP Shilingi 30,000.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Yanga SC pia imewaelekeza mashabiki namna ya kununua tiketi kwa kutumia simu janja au simu za kawaida kwa kupiga *149*46*11# na kufuata maelekezo.

Wananchi sasa wanaelekeza nguvu zao katika kuhakikisha wanaanza hatua ya makundi kwa matokeo mazuri mbele ya MC Alger, huku wakitarajia kupata sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wao.