FIFA yaidhinisha zabuni za pamoja za Kombe la Dunia la Wanawake 2031 na 2035

Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA) limethibitisha kuwa zabuni mbili za pamoja za kuandaa fainali za Kombe la Dunia la Wanawake za mwaka 2031 na 2035 zimekidhi vigezo vya chini vya uandaaji, hivyo kuwasilishwa kwenye mkutano maalumu wa FIFA kwa ajili ya kuidhinishwa.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na FIFA Jumatano, Novemba 11, zabuni ya mwaka 2031 imewasilishwa kwa pamoja na Marekani, Mexico, Costa Rica na Jamaica.

Nchi hizo zimependekeza kutumia viwanja 20 vilivyopo katika miji 20 tofauti na kupata alama 4.4 kati ya tano katika tathmini ya FIFA.

Kwa upande mwingine, zabuni ya mwaka 2035 imewasilishwa kwa pamoja na England, Ireland Kaskazini, Scotland na Wales, ambazo zimependekeza viwanja 19 katika miji 15 ya mwenyeji na kupata alama 4.3 kati ya tano.

FIFA imeeleza kuwa Kombe la Dunia la Wanawake la mwaka 2031 litakuwa la kwanza kutumia mfumo wa timu 48, huku toleo la mwaka 2035 likitarajiwa kuendelea na mfumo huo.

Katika mfumo huo, timu zitagawanywa katika makundi 12 yenye timu nne kila moja, kabla ya kuingia hatua ya mtoano itakayoanzia raundi ya timu 32 bora.

Uamuzi wa mwisho kuhusu zabuni hizo unatarajiwa kufanyika katika mkutano maalumu wa FIFA utakaofanyika Novemba 23.

Wakati huo huo, toleo lijalo la Kombe la Dunia la Wanawake litafanyika nchini Brazil kuanzia Juni 24 hadi Julai 25, 2027.