Mashujaa Queens imefanya mabadiliko katika benchi lake la ufundi baada ya kumtangaza rasmi Kocha Edna Lema ‘Mourinho’ kuwa kocha mkuu mpya wa timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania.
Kupitia taarifa iliyotolewa leo, Novemba 10, 2026, klabu hiyo imemkaribisha kocha huyo ambaye amesaini mkataba wa mwaka mmoja, akipewa jukumu la kuiongoza timu hiyo katika mashindano mbalimbali.
Kibarua cha kwanza cha Edna Lema kinatarajiwa kuwa mchezo dhidi ya Simba Queens utakaochezwa Jumatano, Novemba 11, 2026, katika Uwanja wa KMC Complex, Mwenge jijini Dar es Salaam.
Mashujaa FC imemkaribisha kocha huyo kwa ujumbe uliosema, “Karibu kwenye himaya ya Kishujaa Edna Lema ‘Mourinho’.”
Edna Lema anajiunga na Mashujaa Queens akiwa na leseni ya ukocha ya CAF A, baada ya kuondoka Yanga Princess takribani siku 42 zilizopita.
Kocha huyo aliondoka Yanga Princess baada ya timu hiyo kupoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya wapinzani wao katika mchezo wa nusu fainali ya Ngao ya Jamii, Septemba 30, 2026.
Ujio wake Mashujaa Queens unatajwa kuwa hatua mpya katika safari yake ya ukocha, huku mchezo wake wa kwanza dhidi ya Simba Queens ukiwa mtihani wa awali katika jukumu lake jipya.
Sasa macho ya mashabiki wa soka la wanawake yanaelekezwa kwenye mchezo huo kuona namna Edna Lema atakavyoanza ukurasa wake mpya ndani ya Mashujaa Queens.