Arsène Wenger Kuivamia Fifa, Infantino Kupata Mpinzani Mkali?

Aliyekuwa kocha wa muda mrefu wa Arsenal, Arsène Wenger, anatajwa kuwa kwenye hatua za mwisho za kutafakari uwezekano wa kuwania nafasi ya urais wa Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA), katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Machi 18, 2027, mjini Rabat, Morocco.

Kwa mujibu wa taarifa za vyombo vya habari vya The Telegraph, Sky Sports na Press Association, Wenger amekuwa akishauriwa na baadhi ya viongozi wakubwa wa soka barani Ulaya kuingia kwenye kinyang’anyiro hicho na kujaribu kumng’oa rais wa sasa, Gianni Infantino.

Wenger, ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi wa Maendeleo ya Soka Duniani wa FIFA, amekuwa akitafakari suala hilo kwa wiki kadhaa na sasa analichukulia kwa uzito, ingawa bado hajafanya uamuzi wa mwisho kuhusu kugombea. Wagombea wanatarajiwa kutangaza nia zao kabla ya Novemba 18, 2026.

Msukumo wa kutafuta mgombea wa kumpinga Infantino umetokana na mvutano ndani ya FIFA kufuatia mpango wa kuuza sehemu ya hisa katika biashara zake za kibiashara zinazohusiana na Kombe la Dunia kwa wawekezaji binafsi, mpango uliokumbana na upinzani mkubwa kutoka kwa mashirikisho mbalimbali, likiwemo UEFA.

Wenger alieleza kuwa hakuhusika katika kuandaa mpango huo na alijifunza kuhusu uwepo wake kupitia vyombo vya habari. Baadaye aliunga mkono uamuzi wa kuuondoa, akisisitiza umuhimu wa uwazi, uadilifu na uhuru wa FIFA.

Hata hivyo, safari ya Wenger kuelekea urais wa FIFA haitakuwa rahisi kutokana na Infantino kuendelea kuwa na uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa mashirikisho ya soka barani Afrika, Asia, Amerika Kusini na Oceania.

Ili kugombea nafasi hiyo, mgombea anatakiwa kupata uteuzi kutoka angalau vyama vitano vya soka vinavyoshiriki FIFA. Tayari aliyekuwa Rais wa Shirikisho la Soka la Japan, Kozo Tashima, ametangaza nia ya kuwania nafasi hiyo.

Wenger, mwenye historia ya miaka 22 ya kuinoa Arsenal, ambako alishinda mataji matatu ya Ligi Kuu England na saba ya Kombe la FA, sasa anaweza kuingia kwenye moja ya mitihani mikubwa zaidi ya uongozi katika maisha yake ya soka.