Yanga SC: Tumepoteza vs Simba SC kwa bahati mbaya

UONGOZI wa Yanga SC, umeweka wazi kuwa umepoteza mchezo wa Kariakoo Dabi kwa bahati mbaya walipokutana kwenye mzunguko wa kwanza.

Oktoba 10,2026 baada ya dakika 90 ubao wa Uwanja wa Uhuru ulisoma Simba SC 2-1 Yanga SC. Mabao yalifungwa na Peter Shalulile dakika ya 5 kwa Yanga SC huku Neo Maema akifunga dakika ya 68 na Ellie Mpanzu dakika ya 71.

Ali Kamwe, Meneja wa Habari na Mawasiliano Yanga SC amesema: “Mwishoni mwa wiki iliyopita, tulicheza mchezo wa Ligi Kuu ya NBC dhidi ya wapinzani wetu wa jadi Simba SC, katika mchezo wa Kariakoo Derby. Kwa bahati mbaya, Young Africans Sports Club tulipoteza mchezo huo kwa mabao mawili kwa moja (2–1).

“Ulikuwa mchezo mzuri, lakini mwisho wa dakika 90, hatukuweza kupata matokeo tuliyoyatarajia. Matokeo yake tukakosa pointi tatu na kupoteza mchezo huo muhimu.

“Kwa kawaida, kupoteza mchezo wa derby kuna tofauti kubwa na kupoteza mchezo mwingine wa ligi. Unapofungwa na timu yoyote, unapoteza pointi tatu lakini unapofungwa na mpinzani wako wa karibu, ambaye mnashindania ubingwa na ambaye ni mtani wako wa jadi, hisia na maumivu huwa tofauti kabisa.

“Tusijidanganye kwa kusema kwamba kufungwa derby ni sawa na kufungwa na timu nyingine yoyote. Hisia zake ni tofauti kwa sababu derby ni sehemu ya maisha yetu.Derby imeunganisha familia, shule, mitaa na maeneo ya kazi.

“Katika mazingira yetu, utani wa Simba na Yanga upo kila mahali. Kwa hiyo, timu yako inapopoteza derby, unakutana na utani na maneno ya hapa na pale kutoka kwa wapinzani wako. Hali hiyo ndiyo inayofanya maumivu ya kushindwa katika mchezo huu kuwa makubwa zaidi.

“Kwa sababu hiyo, nichukue nafasi hii kuwapa pole mashabiki na wanachama wenzangu wa Yanga ambao tuliumizwa na matokeo ya mchezo huo. Tunatambua hisia zenu, hasira zenu na namna ambavyo matokeo yale yamewapokelewa na wengi wetu.Hata hivyo, ni muhimu kutambua kwamba katika soka ushindi na kushindwa ni sehemu ya mchezo. Jambo la msingi ni namna tunavyopokea matokeo na kujipanga upya kwa ajili ya changamoto zinazofuata,” .