Rwanda imeingia katika historia ya maandalizi ya michezo barani Afrika baada ya kusaini mkataba wa miaka 10 na mashindano ya Formula 1 wa kuandaa mbio hizo nchini humo kuanzia mwanzoni mwa miaka ya 2030.
Mashindano hayo, yanayotarajiwa kuitwa African Grand Prix, yatafanyika katika uwanja mpya wa kisasa wa mbio unaojengwa eneo la Bugesera, takriban kilomita 40 kusini mwa mji mkuu wa Kigali, karibu na Uwanja Mpya wa Kimataifa wa Ndege wa Kigali.
Ujio wa mashindano hayo utakuwa hatua muhimu kwa Afrika, kwani bara hilo halijaandaa mbio za Formula 1 tangu mwaka 1993, wakati mashindano hayo yalipofanyika nchini Afrika Kusini.
Kwa mujibu wa taarifa ya Formula 1, mradi huo umetokana na miaka kadhaa ya ushirikiano uliolenga kuweka msingi wa kuandaa mashindano yenye mafanikio, endelevu na yanayokidhi viwango vya kimataifa kwa muda mrefu.
Uwanja huo umebuniwa na Alex Wurz, dereva wa zamani wa Formula 1, kwa kuzingatia mandhari ya asili ya eneo la Bugesera.
Ubunifu wake umetumia tofauti za mwinuko wa ardhi kuunda changamoto za kipekee kwa madereva, huku ukilenga kuwapa mashabiki nafasi nzuri ya kutazama mbio hizo.
Mradi huo ni sehemu ya juhudi za Rwanda kujitangaza kimataifa kupitia uwekezaji katika miundombinu na kuandaa matukio makubwa ya michezo.
Formula 1 kulenga kukuza soko la Afrika
Formula 1 inatarajia kuwa kurejea kwa mashindano hayo barani Afrika kutasaidia kuongeza umaarufu wa mchezo huo katika bara ambalo bado halijatumika kikamilifu kama soko la mashindano hayo ikilinganishwa na Ulaya, Asia na Amerika.
Hata hivyo, pamoja na kusainiwa kwa mkataba huo, bado haijafahamika ni mwaka gani hasa African Grand Prix itajumuishwa rasmi katika kalenda ya mashindano ya Formula 1.
Rwanda yakabiliwa na mjadala kuhusu matumizi ya michezo
Pamoja na matarajio ya kiuchumi na kimichezo yanayohusishwa na mradi huo, hatua ya Rwanda kuandaa mashindano makubwa ya kimataifa inaweza pia kuibua mjadala kuhusu matumizi ya matukio ya michezo kuboresha taswira ya nchi duniani.
Rwanda imewahi kukabiliwa na tuhuma za kutumia matukio makubwa ya michezo kwa lengo hilo, madai ambayo serikali yake imekuwa ikiyakanusha.
Hata hivyo, maandalizi ya African Grand Prix yanaweka Rwanda katika nafasi ya kuwa miongoni mwa nchi zinazotafuta kuvutia uwekezaji, watalii na mashabiki wa michezo kupitia mashindano ya kimataifa.