Yanga Yapata Pigo, Duke Abuya Aumia Paja

Yanga SC inaweza kumkosa kiungo wake, Duke Abuya, kwa kipindi ambacho bado hakijafahamika baada ya kupata jeraha la nyama za paja katika mchezo wa watani wa jadi dhidi ya Simba SC, ambao Yanga ilipoteza kwa mabao 2-1.

Taarifa kuhusu hali ya mchezaji huyo imetolewa na Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Yanga, Ally Kamwe, aliyesema daktari wa klabu hiyo, Moses Etutu, amethibitisha kuwa Abuya ameumia, ingawa tathmini ya awali haijaweka wazi ukubwa wa jeraha hilo.

Kamwe ameeleza kuwa uchunguzi wa kina umepangwa kufanyika leo ili kubaini hali halisi ya kiungo huyo na muda anaoweza kuhitaji kurejea uwanjani.

Abuya alipata majeraha hayo wakati wa mchezo huo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, kufuatia faulo aliyofanyiwa na winga wa Simba, Libase Gueye.

Kiungo huyo alipewa matibabu na kujaribu kurejea mchezoni, lakini alishindwa kuendelea kutokana na hali yake, hivyo benchi la ufundi la Yanga kufanya mabadiliko dakika ya 25 kwa kumtoa na kumuingiza Fredy Ngoma.

Hadi sasa, Yanga inasubiri matokeo ya uchunguzi wa kitabibu yatakayobainisha kiwango cha jeraha hilo na uwezekano wa Abuya kurejea katika michezo ijayo.