Mwanachama wa Klabu ya Yanga, Haji Omari Ramadhani Mpili, amezikwa leo Jumatatu, Septemba 28, 2026, katika Makaburi ya Msikiti Mkuu, Wilaya ya Ikwiriri, Mkoa wa Pwani.
Maziko hayo yamefanyika majira ya saa 10:00 jioni, kufuatia kifo cha Haji Mpili kilichotokea usiku wa Jumapili, Septemba 27, 2026, akiwa anapatiwa matibabu katika Kituo cha Afya cha Wilaya ya Ikwiriri.
Katika msiba huo, Msemaji wa Yanga, Ally Kamwe, amewasili nyumbani kwa marehemu Ikwiriri na kushiriki kutoa pole kwa familia, ndugu na jamaa wa marehemu.
Akizungumza wakati wa msiba, mtoto wa Haji Mpili ametoa shukrani kwa Rais wa Yanga kwa namna alivyomhudumia baba yake wakati wa kipindi cha ugonjwa hadi alipofariki dunia.
Maziko hayo yamehudhuriwa na ndugu, jamaa, marafiki pamoja na baadhi ya wanachama na wapenzi wa Yanga waliofika kutoa heshima zao za mwisho kwa marehemu.
Haji Omari Ramadhani Mpili alifariki dunia usiku wa Septemba 27, 2026, akiwa anapatiwa matibabu katika Kituo cha Afya cha Wilaya ya Ikwiriri.
Uongozi wa Yanga uliwasilisha salamu za pole kwa familia, ndugu, jamaa, marafiki na wadau wa soka kufuatia kifo cha mwanachama huyo.
