Msemaji wa Timu za Taifa za Tanzania, Haji Manara, amezitaka klabu zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania kuwapa nafasi zaidi wachezaji vijana katika vikosi vya kwanza ili kuwajengea uzoefu, kuongeza kiwango chao na kuwaandaa kwa ajili ya kuitumikia timu za taifa.
Manara amesema hatua hiyo itawasaidia vijana hao kuimarika zaidi na kuwa na uwezo wa kushindana katika mashindano ya kimataifa pindi wanapoitwa kwenye timu za taifa.
Amesema mafanikio ya Ngorongoro Heroes kufuzu Fainali za AFCON U20 mwaka 2027 nchini Ghana ni ishara ya umuhimu wa kuwaandaa vijana katika mazingira bora ya ushindani.
Akitolea mfano mabeki wa kati wa Ngorongoro Heroes, Manara amesema kupata muda wa kutosha wa kucheza katika klabu zao kumewasaidia kuimarika na kutoa mchango mkubwa wanapoungana na timu ya taifa.
Ngorongoro Heroes imefuzu Fainali za AFCON U20 baada ya kuifunga Burundi mabao 2-0 katika mchezo wa nusu fainali ya CECAFA uliochezwa Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam.
Kikosi hicho kinatarajiwa kukutana na Sudan katika mchezo wa fainali utakaochezwa Alhamisi, Septemba 24, 2026.
Manara amewapongeza wachezaji wa Ngorongoro Heroes kwa kiwango walichoonesha hadi kufikia hatua hiyo, huku akieleza matumaini ya kufanya vizuri katika mchezo wa fainali.