Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imetoa ufafanuzi kuhusu jezi za timu za taifa kufuatia mjadala uliotokana na mchakato wa kuzibadilisha na kuishirikisha Wizara katika maelekezo yaliyotolewa mwezi Februari 2026.
Katika taarifa yake ya Septemba 18, 2026, Wizara imesema Serikali inaendelea kuweka fedha nyingi katika maandalizi ya timu za taifa zinazoshiriki mashindano ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na maandalizi ya Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano makubwa ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027, hivyo kuna umuhimu wa kuboresha jezi za timu za taifa ili ziakisi manufaa kwa nchi.
Wizara pia imesema, sambamba na kutambua utambulisho wa jezi hizo, Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Christian Makonda, ameunda Kamati ya kuchunguza mikataba ya wazabuni wa jezi hizo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kamati hiyo itachunguza mikataba ya wazabuni pamoja na manufaa yanayotokana na mikataba hiyo kwa timu za taifa, ikiwemo namna Serikali inavyoweza kupata fursa ya mauzo ya jezi yanayopaswa kuchangia katika uendeshaji wa timu za taifa.
Taarifa hiyo imetolewa na Zaituni Mkwama, Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, kwa niaba ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Septemba 18, 2026.
