Ibraheem Jabaar atozwa milioni 5 kisa kiwiko

Kamati ya Uendeshaji na Usimamizi ya Bodi ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB) imemtoza faini ya Sh milioni 5 mchezaji wa Simba SC, Ibraheem Jabaar, kwa kosa la kumpiga kiwiko mchezaji wa Pamba Jiji FC, Abdulkarim Iddy.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi iliyotolewa na TPLB, mbali na faini hiyo, adhabu ya kadi nyekundu aliyoonyeshwa Jabaar kutokana na tukio hilo itaendelea kubaki kama ilivyo.

Jabaar alionyeshwa kadi nyekundu dakika ya 44 katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa CCM Kirumba, ambapo baada ya dakika 90 ubao ulisoma Pamba Jiji FC 1-2 Simba SC.

Mbali na adhabu hiyo kwa mchezaji, Simba SC pia imetozwa faini ya Sh milioni 5 kutokana na kosa la mashabiki wake kuwarushia chupa waamuzi wakati wa mchezo huo.

Hivyo, mchezo wa Pamba Jiji FC dhidi ya Simba SC umeigharimu klabu hiyo jumla ya Sh milioni 10 kutokana na makosa yaliyotokea ndani na nje ya uwanja.

Katika adhabu nyingine, TPLB imeitaja pia mechi ya Pamba Jiji FC dhidi ya Dodoma Jiji FC, iliyomalizika kwa sare ya 1-1, ambapo Dodoma Jiji imetozwa faini ya Sh milioni 5 kwa kosa la wachezaji wake kuonekana wakifanya vitendo vinavyoashiria imani za kishirikina kuelekea mchezo huo.

Kwa upande mwingine, Namungo FC imepewa adhabu ya faini ya Sh milioni 5 kwa kosa la vijana waokota mipira (Ball Boys) kuficha mipira na wakati mwingine kuchelewa kuitafuta baada ya mipira kutoka nje ya uwanja.

Kamati imeeleza kuwa kitendo hicho kinakiuka kanuni za mchezo na kinaweza kuathiri mwenendo wa mchezo.

Kwa ujumla, adhabu hizo zinaendelea kuwakumbusha wachezaji, vilabu na mashabiki umuhimu wa kuzingatia kanuni na nidhamu wakati wa michezo ya Ligi Kuu Tanzania.