Lionel Messi ametwaa tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka (Best Soccer Player) kwenye Tuzo za ESPY 2026, baada ya kuwashinda nyota wengine watatu waliokuwa kwenye orodha ya wanaowania tuzo hiyo; Ousmane Dembélé wa PSG na Ufaransa, Alexia Putellas wa Barcelona na Hispania, pamoja na Temwa Chawinga wa KC Current na Malawi.
Tuzo hiyo ilitangazwa usiku wa kuamkia Julai 16, 2026 katika hafla ya ESPY Awards iliyofanyika ndani ya ukumbi wa David H. Koch Theater uliopo Lincoln Center, jijini New York, ambapo mastaa wa michezo kutoka mataifa mbalimbali walikusanyika kusherehekea mafanikio ya mwaka uliopita.
Ushindi wa Messi umeongeza furaha kwa nahodha huyo wa Inter Miami, ukija saa chache baada ya kuiongoza Argentina kutinga fainali ya Kombe la Dunia 2026 kwa kutoa pasi mbili za mabao katika ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya England kwenye hatua ya nusu fainali.