JKT Tanzania Wamjulia Hali Pacome, Wahabi Aomba Dua

Mchezaji wa JKT Tanzania FC, Hassan Wahabi, leo amefika katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam na kuongoza dua ya kumuombea kiungo wa Yanga SC, Pacome Zouzoua, aliyelazwa kutokana na maumivu aliyoyapata katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara kati ya JKT Tanzania na Yanga SC.

Wahabi, ambaye bila kukusudia alihusika katika tukio lililosababisha majeraha hayo wakati wakigombea mpira, alifika hospitalini akiwa ameongozana na Afisa Mtendaji Mkuu wa JKT Tanzania FC, Meja Stan Chahe, pamoja na Afisa Habari na Mawasiliano, Masau Kuliga Bwire.

Ujumbe huo ulimjulia hali Pacome na kumtakia uponaji wa haraka, huku wakisisitiza mshikamano na uhusiano mzuri kati ya klabu hizo mbili.

Akizungumza akiwa hospitalini, Pacome Zouzoua alimueleza Wahabi kuwa hana kinyongo na tukio hilo, akisisitiza kuwa majeraha ni sehemu ya mchezo wa soka na yanatokea bila kukusudiwa.

Naye mchezaji wa zamani wa Yanga SC, Aziz Ki, alieleza kuwa tukio hilo ni changamoto ya kawaida katika soka na kumtaka Wahabi kuendelea na majukumu yake kwa utulivu na amani.

Kwa upande wake, Rais wa Yanga SC, Eng. Hersi Said, amesema tukio hilo linapaswa kusahaulika na kuachwa nyuma, huku akiwataka wadau wa soka kuendelea kumuombea Pacome apone haraka na kurejea uwanjani akiwa na nguvu zaidi.

Aidha, mlezi na mdhamini mkuu wa Yanga SC, Ghalib Said Mohamed (GSM), amepongeza kitendo cha uungwana kilichoonyeshwa na uongozi wa JKT Tanzania pamoja na mchezaji Wahabi, akisema ni mfano mzuri wa maadili ya michezo na mshikamano kati ya klabu.

GSM amesisitiza kuwa tukio hilo halikuwa la makusudi bali ni bahati mbaya ya mchezo wa soka, na akawataka wadau wote kuendelea kudumisha amani na heshima ndani na nje ya uwanja.