Australia imeanza vyema kampeni yake ya Kombe la Dunia baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Uturuki katika mchezo wa Kundi D uliochezwa Vancouver usiku wa Jumamosi.
Nyota kijana Nestory Irankunda aliifungia Australia bao la kwanza dakika ya 27 kwa shuti la chini lililowashinda mabeki watatu wa Uturuki waliokuwa wakimkaba. Baada ya kufunga, Irankunda alisherehekea kwa kupiga bendera ya kona ikiwa ni heshima kwa gwiji wa soka la Australia, Tim Cahill.
Kwa kufanya hivyo, mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 20 anayekipiga katika klabu ya Watford aliandika historia kwa kuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kuifungia Australia bao katika Kombe la Dunia.
Mlinda mlango Patrick Beach alikuwa nyota mwingine wa mchezo huo baada ya kuokoa mashuti manane hatari ya Uturuki. Beach alipewa nafasi ya kuanza kikosini badala ya kipa mkongwe Matthew Ryan katika uamuzi uliowashangaza wengi kutoka kwa kocha Tony Popovic.
Uturuki, iliyorejea katika Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza tangu mwaka 2002, ilijaribu kusawazisha kupitia nyota wake Arda Güler na Kenan Yildiz, lakini ilishindwa kuvunja ukuta wa Australia.
Connor Metcalfe aliihakikishia Australia ushindi dakika ya 75 baada ya kutumia makosa ya Ismail Yüksek na kufunga bao la pili lililozima matumaini ya Uturuki kurejea mchezoni.
Ushindi huo unaifanya Australia kuanza vyema safari yake ya Kombe la Dunia, huku Uturuki ikilazimika kutafuta matokeo mazuri katika michezo ijayo ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kusonga mbele.
Katika Kundi D, Australia na Uturuki zipo pamoja na Marekani na Paraguay. Marekani tayari imeonyesha ubabe wake baada ya kuichapa Paraguay mabao 4-1 katika mchezo wao wa kwanza.