FIFA Kuilipa Pyramids FC Baada ya Uteuzi wa Mayele World Cup 2026

Uteuzi wa Fiston Mayele katika kikosi cha DR Congo national football team kitakachoshiriki FIFA World Cup 2026 umetarajiwa kunufaisha klabu yake ya Pyramids FC kwa mapato ya takribani dola 198,000 (sawa na Shilingi milioni 514) kutoka FIFA.

Kwa mujibu wa taarifa hizo, FIFA hulipa klabu ambazo wachezaji wake wanashiriki Kombe la Dunia, ambapo kila siku mchezaji akiwa kwenye michuano hiyo huingizia klabu yake takribani dola 11,000.

Kwa kuwa DR Congo inatarajiwa kuwepo kambini na kucheza kwa angalau siku 18 kuanzia maandalizi hadi hatua ya makundi, Pyramids FC inatarajiwa kunufaika moja kwa moja kupitia uwepo wa Mayele katika mashindano hayo.

Kiasi hicho kinaweza kuongezeka iwapo DR Congo itafanikiwa kusonga mbele zaidi katika hatua za mtoano, jambo litakalozidisha muda wa Mayele kubaki kwenye michuano hiyo.

Mayele ni miongoni mwa washambuliaji waliochaguliwa na kocha Sébastien Desabre, ambaye ana matumaini makubwa na kikosi hicho katika mashindano ya Kombe la Dunia 2026 yatakayofanyika Marekani, Canada na Mexico.