Tyson na Mayweather Kupigana DR Congo, Pambano la Maonyesho Kuvuta Hisia za Dunia

Magwiji wa ndondi, Mike Tyson na Floyd Mayweather Jr., wanatarajiwa kukutana katika pambano la maonyesho litakalofanyika Aprili 4, 2026 nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).

Pambano hilo linatajwa kuwa la kihistoria, likirejesha kumbukumbu za mapambano makubwa yaliyowahi kufanyika barani Afrika, hususan tukio maarufu la Rumble in the Jungle lililowakutanisha Muhammad Ali na George Foreman mwaka 1974 mjini Kinshasa, wakati huo ikiitwa Zaire chini ya utawala wa Rais Mobutu Sese Seko.

Mabingwa wa Enzi Tofauti Wakutanapo

Tyson (59) aliwahi kuwa bingwa wa dunia wa uzani wa juu na ni miongoni mwa mabondia waliotawala miaka ya 1980 kwa kasi na nguvu kubwa ya kupiga. Ingawa alistaafu muda mrefu uliopita, ameendelea kushiriki mapambano ya maonyesho, ikiwemo pambano lake la mwaka 2024 dhidi ya Jake Paul lililovutia watazamaji takribani milioni 100 duniani.

Kwa upande mwingine, Mayweather (48) alistaafu ndondi akiwa hajapoteza pambano hata moja katika taaluma yake ya kulipwa. Alitwaa mataji ya dunia katika uzani tofauti na kujijengea rekodi ya kipekee ya ushindi mfululizo bila kupigwa.

Pambano la Maonyesho Leneye Uzito wa Kihistoria

Ingawa ni pambano la maonyesho, tukio hili linatarajiwa kuvuta hisia kubwa kimataifa kutokana na hadhi ya mabondia hao wawili. Wengi wanaona ni mkutano wa mastaa waliotawala enzi tofauti, huku Afrika ikirejea tena kuwa kitovu cha tukio kubwa la ndondi duniani.

Waandaaji wa pambano hilo wanatarajiwa kutangaza rasmi ukumbi utakaotumika pamoja na maelezo ya ziada kuhusu ratiba ya maandalizi katika wiki zijazo.