Matumaini ya wawakilishi wa Tanzania, Young Africans (Yanga SC), kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAFCL) yamepata pigo zito baada ya kukubali kichapo cha bao 1-0 dhidi ya AS FAR Rabat katika mchezo mkali uliopigwa dimba la Olympique de Rabat, Morocco.
Yanga walionyesha nidhamu kubwa ya kujilinda kwa muda mrefu wa mchezo huo, wakizuia mashambulizi kadhaa ya wenyeji, lakini presha ya AS FAR iliendelea kuongezeka kadri dakika zilivyoyoyoma.
Pigo lilikuja dakika za lala salama, ambapo Anas Bach alifunga dakika ya 85, akimalizia shambulio lililowapa wenyeji bao muhimu lililobadilisha kabisa mwelekeo wa mchezo na kuzima ndoto za Yanga kuondoka na pointi ugenini.
Matokeo hayo yanaifanya Yanga kubaki katika nafasi ngumu kwenye kundi B, wakihitaji ushindi katika michezo iliyosalia ili kufufua matumaini ya kusonga mbele.
Katika mchezo mwingine wa kundi hilo, JS Kabylie walitoka sare tasa ya 0-0 dhidi ya mabingwa watetezi Al Ahly, matokeo yaliyozidi kuifanya presha iongezeke kwa timu zote zinazowania nafasi mbili za juu.
Matokeo Kamili
FT: AS FAR Rabat 🇲🇦 1-0 🇹🇿 Yanga SC
⚽ 85’ Anas Bach
FT: JS Kabylie 🇩🇿 0-0 🇪🇬 Al Ahly
Msimamo Kundi B
-
Al Ahly – 9 pts (+5)
-
AS FAR – 8 pts (+1)
-
Yanga SC – 5 pts (-2)
-
JS Kabylie – 3 pts (-4)
Kwa matokeo hayo, Yanga sasa wanalazimika kupambana kufa na kupona katika mechi zilizobaki kama wanataka kufuzu, huku kila pointi ikiwa ya thamani kubwa zaidi.