Ndege ya Turkish Airlines aina ya Airbus A321 iliyokuwa ikifanya safari kuelekea Barcelona ililazimika kutua kwa dharura katika Uwanja wa Ndege wa Barcelona–El Prat, baada ya abiria mmoja kuunda jina la Wi‑Fi hotspot lenye ujumbe wa kutishia bomu siku ya Januari 15, 2026.
Ndege hiyo, yenye namba ya safari TK1853, ilikuwa imeruka kutoka Istanbul ikiwa na abiria 148 pamoja na wafanyakazi saba. Tukio hilo lilizua taharuki baada ya ujumbe uliosomeka “I have a bomb, everyone will die” kuonekana kupitia mtandao wa Wi‑Fi ndani ya ndege.
Kutokana na tishio hilo, ndege hiyo iliandamwa na ndege za kivita za NATO kama hatua ya kiusalama kabla ya kutua kwa dharura katika uwanja wa Barcelona-El Prat.
Baada ya kutua, vyombo vya usalama vilifanya ukaguzi wa kina lakini hakuna kitu chochote hatari kilichobainika. Abiria aliyekuwa amehusika na uundaji wa ujumbe huo alitambuliwa na kukamatwa na polisi kwa ajili ya kuhojiwa zaidi.