Gabon Yaondoa Adhabu Dhidi ya Aubameyang na Timu ya Taifa

Shirikisho la soka la Gabon limetangaza kuwa hatua zilizochukuliwa dhidi ya timu ya taifa na wachezaji akiwemo Pierre-Emerick Aubameyang baada ya kutoka mapema katika michuano ya Kombe la Mataifa ya Afrika zimeondolewa.

Katika michuano hiyo inayofanyika nchini Morocco, Gabon ilipoteza mechi zote za Kundi F kwenye kombe la mataifa ya Afrika 2025, ambapo ilimenyana na Cameroon, Msumbiji na Côte d’Ivoire.

Hii ilisababisha Waziri wa Michezo, Paul Ulrich Kessany, kutangaza kwenye televisheni kwamba timu ya taifa imesimamishwa, pamoja na uamuzi uliochukuliwa dhidi ya nahodha wake, Pierre-Emerick Aubameyang, na mlinzi Bruno Ecuele Manga.

Shirikisho la Soka la Gabon sasa limetangaza kuwa uamuzi huo umeondolewa kwa sababu ungesababisha nchi hiyo kusimamishwa na FIFA kwa kuingilia kisiasa katika maamuzi ya soka.

Shirikisho la soka nchini Gabon liliongeza kuwa lengo lao kuu sasa ni maandalizi ya Kombe la Mataifa ya Afrika 2027 itakayofanyika Tanzania, Uganda na Kenya.