>

SIMBA YAKIRI WAPINZANI WAO KIMATAIFA SIO WANYONGE

UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa wapinzani wao kwenye Kombe la Shirikisho Afrika sio wanyonge hivyo watawakabili kwa tahadhari kupata matokeo chanya kwenye mchezo unaotarajiwa kuchezwa Septemba 15 2024 nchini Libya.

Tayari msafara wa Simba umeanza safari kuwafuata wapinzani wao ambapo Septemba 11 mapema kikosi kilikwea pipa kutoka Bongo na kuweka kambi Uturuki na mapema Septemba 12 kimeanza safari kuelekea Libya na kinatarajiwa kuwasili leo kuanza maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo huo.

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba, amesema kuwa wanatambua upinzani ni mkubwa na wapinzani wao Al Ahly Tripoli ni miongoni mwa timu zenye mafanikio nchini Libya hivyo wana kazi kubwa ya kufanya kutafuta ushindi kwenye mchezo huo.

“Wanasimba wanapaswa kutambua kwamba tunakwenda kucheza na Ahly Tripoli ambayo  ni klabu ya pili kwa mafanikio Libya lakini ndio klabu yenye mafanikio zaidi kimataifa nchini kwao. Mafanikio yao makubwa ni kucheza nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la Afrika 2022 na robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika 2017.

“Msimu uliopita walimaliza nafasi ya tatu, Kufuatia kutoridhishwa na matokeo hayo, wakafanya usajili mkubwa ili kurejesha heshima yao. Miongoni mwa usajili wa kushtua waliofanya ni Mabolulu ambae amesajiliwa kwa dau la bilioni 4 na inatajwa kuwa ndio usajili mkubwa zaidi katika historia ya klabu hiyo

“Mechi ya kwanza ni Septemba 15, mechi hii ya ugenini tunawategemea zaidi wachezaji wetu wapambane kadri ya uwezo wao.
Mechi ya pili ni Septemba 22 Benjamin Mkapa hii inatutegemea sisi mashabiki kuipeleka Simba yetu hatua ya makundi. Tupo tayari kwa ushidani na tunaamini mchezo utakuwa na ushindani mkubwa.”