KAZI imeanza kwa wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania,Taifa Stars kwa ajili ya maandalizi ya michezo miwili ya kujiandaa kufuzu AFCON 2025.
Taifa Stars, chini ya Kaimu Kocha Mkuu Hemed Morocco tayari wachezaji wameingia kambini baada ya kukamilisha majukumu yao kutoka kwenye timu ambazo zinashiriki Ligi Kuu Bara Tanzania.
Agosti 29 2024 Kikosi cha Taifa Stars klianza mazoezi kwenye Uwanja wa Gymkhana, Dar es Salaam kujiandaa na michezo hiyo miwili ya kufuzu AFCON 2025 dhidi ya Ethiopia na Guinea itakayochezwa Septemba 4 na Septemba 10, 2024
Agosti 30 kikosi cha Stars kimefanya mazoezi mapema kwenye Uwanja wa KMC, uliopo Mwenge ikiwa ni mwendelezo wa mazoezi ya timu hiyo ya taifa ili ipate matokeo mazuri kwenye michezo hiyo miwili.
Kiungo wa Stars, Feisal Salum ameweka wazi kuwa wapo tayari kwa ajili ya mechi hizo hivyo mashabiki wajitokeze kwa wingi Septemba 4 2024 Uwanja wa Mkapa kushuhudia mchezo wao dhidi ya Ethiopia.
Morocco amesema kuwa wachezaji wote wapo tayari kwa michezo hiyo huku ripoti kutoka kwa wataalamu wa afya ikiweka wazi kuwa wachezaji wote wapo fiti.
“Ripoti kutoka kwa daktari inaeleza kuwa wachezaji wote wapo fiti kwa ajili ya michezo yetu hivyo ni maandalizi na utayari kuelekea kwenye mechi zetu ambazo zitakuwa na ushindani mkubwa.”