>

YANGA: HAIKUWA RAHISI KUVUNA POINTI TATU ZA KAGERA

UONGOZI wa Yanga umeweka wazi kuwa haikuwa rahisi kuvuna pointi tatu muhimu mbele ya Kagera Sugar kwenye mchezo wa kwanza ndani ya msimu wa 2024/25.

Ipo wazi kwamba mchezo wao wa msimu wa 2023/24 walipocheza Kaitaba baada ya dakika 90 ubao ulisoma Kager Sugar 0-0 Yanga hivyo mabingwa hao watetezi waligawana pointi mojamoja na Kagera Sugar.

Katika mchezo wa 2024/25 uliochezwa Uwanja wa Kaitaba baada ya dakika 90 ubao ulisoma Kagera Sugar 0-2 Yanga huku mabao yakifungwa na Maxi Nzengeli dakika ya 25 na Clement Mzize dakika ya 88.

Walter Harrison, Meneja wa Yanga ameweka wazi kuwa kuanza kwa ushindi ni jambo la kumshukuru Mungu kwa kuwa mchezo ulikuwa mgumu na kla timu ilikuwa inapambana kupata matokeo.

“Tunamshukuru Mungu kupata matokeo mazuri kwenye mchezo wetu dhidi ya Kagera Sugar. Haikuwa rahisi unaona namna kila timu ilivyokuwa ikionyesha ushindani na mwisho tumepata matokeo mazuri.

“Pointi tatu muhimu kwetu zinatupa nguvu ya kuwa kwenye mwanzo mzuri hivyo tunawapongeza wachezaji kwa kazi kubwa waliyofanya pamoja na mashabiki kujitokeza kwa wingi.”