>

SIMBA YATOA TAMKO KUHUSU KAGOMA

UONGOZI wa Simba umeweka wazi kuwa upo bega kwa bega na mchezaji wao Yusuph Kagoma na unatamba naye kwa kuwa anasifa zote za kuwa katika kikosi hicho kinachonolewa na Kocha Mkuu, Fadlu Davids.

Mechi mbili za Ligi Kuu Bara Fadlu ameongoza na kuhushudia kikosi hicho kikipata ushindi kwenye mchezo dhidi ya Tabora United kwa mabao 3-0 na mchezo wa pili ilikuwa Simba 4-0 Fountain Gate.

Mchezo wa kwanza wa ushindani kwa Kagoma ingizo jipya ndani ya Simba akiwa na uzi wa Simba kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara ilikuwa dhidi ya Fountain Gate, Uwanja wa KMC, Mwenge.

Ahmed Ally, Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema kuwa wachezaji waliopo kwenye kikosi cha Simba wanajituma katika kutimiza majukumu yao huku wakifurahia burudani kutoka kwa Kagoma.

“Kagoma tupo naye na tunatamba naye Wanasimba kwa kuwa hii ni mashine ya kazi na kuna mengi yanakuja. Furaha kubwa kuona matokeo yanapatikana uwanjani kwani msimu huu ni ubaya ubwela.”