Home International REBECCA REFA MWENYE REKODI YAKE EPL

REBECCA REFA MWENYE REKODI YAKE EPL

REBECCA Welch, ameweka rekodi ya kuwa mwamuzi wa kwanza mwanamke kuchezesha mechi ya Premier League, alifanya hivyo katika mchezo baina ya Fulham dhidi ya Burnley, Jumamosi iliyopita.

Welch kwa muda mrefu amekuwa akijihusisha na soka la wanaume, ambapo kwanza aliweka rekodi ya kuwa mwamuzi wa kwanza wa kike kuchezesha mechi ya EFL, Aprili 2021, kisha Kombe la FA la wanaume, Januari 2022.

Pia Welch alichaguliwa kuwa mwamuzi wa akiba katika mchezo wa Premier ambao Manchester United iliibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Fulham, Novemba 2023 na kuwa mwamuzi wa kwanza mwanamke kufanya hivyo katika ligi hiyo.

Akiwa na miaka 40, huko nyuma aliwahi kuchezesha mechi za National League, huku pia akiwa anachezesha mechi za Ligi Kuu ya Wanawake England. Mwaka huu alikuwepo katika michuano ya Kombe la Dunia Wanawake.

Chini ya mkongwe, Howard Webb, Bodi ya PGMOL inayosimamia waamuzi, imeonekana kuja na mabadiliko makubwa sana.

Katika mabadiliko hayo, yamemfanya pia Sam Allison kuwa mwamuzi wa kwanza mweusi kuchezesha mechi ya Premier League tangu Uriah Rennie afanye hivyo mwaka 2008. Allison atachezesha mechi kati ya Sheffield United dhidi ya Luton, leo Jumanne.

Wakati Welch akiweka rekodi hiyo, Wendy Toms aliweka rekodi ya kuwa mwanamke wa kwanza kuwa mwamuzi wa akiba katika ligi ya ngazi ya juu England mwaka 1997, baadaye wakaja Amy Fearn, Sian Massey-Ellis na Natalie Aspinall.

Katika michuano ya Kombe la Dunia Wanawake 2023, Welch alichezesha mechi tatu ikiwemo ya hatua ya 16 bora kati ya Australia dhidi ya Denmark.

Rekodi zinaonesha kwamba, Welch alichezesha fainali ya Kombe la FA Wanawake mwaka 2017 na 2020, kabla ya kupandishwa ngazi ya UEFA kwa waamuzi wa kike mwaka uliofuatia baada ya kuacha kazi yake ya uuguzi.

Mwaka 2021, alikuwa mwanamke wa kwanza kuchezesha mechi ya kimashindano ya wanaume nchini England iliyozikutanisha Port Vale na Harrogate Town katika michuano ya League Two.

Webb ameuzungumzia uchaguzi huo wa Welch na Allison akisema: “Ninajisikia furaha kuchaguliwa kwa Rebecca Welch kuwa mwamuzi wa kwanza mwanamke kuchezesha Premier League, katika Boxing Day,”.

Previous articleUKIZUBAA HUNA CHAKO TATU BORA/ YANGA YAZICHAPA ZOTE
Next articleAACHWE AONDOKE SIMBA CLATOUS CHAMA/SURA YA PILI YA KOCHA