DESEMBA INAFUNGULIWA KWA KAZI KIMATAIFA

    GHAFLA yule uliyempa ahadi utamlipa Desemba, ngoma hii hapa imeshafika kazi kukamilisha madeni kwa wakati. Weka kando hilo, kwa wawakilishi wa kimataifa kuna shughuli nzito kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.

    Madeni yote waliyoahidi kuyalipa leo Desemba 2 kwa nyakati tofauti kila mmoja atakuwa na dakika 90 za kulipa mmoja atakuwa nyumbani na mwingine huko ugenini kukamilisha kazi yake.

    Hapa tunakuletea namna Desemba inafunguliwa na kazi kimataifa:-

    Ugenini kuchungu

    Chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi, Yanga ilifungua pazia kwenye mechi za Ligi ya Mabingwa hatua ya makundi. Ilikuwa ni Novemba 24 wachezaji walishuhudia ubao ukisoma CR Belouizdad 3-0 Yanga. Ilikuwa ni siku mbaya kazini.

    Licha ya Yanga kuwa ugenini na kumiliki mpira kwa asilimia kubwa walichovuna ni maumivu kwa kuwa waliacha pointi tatu mazima ugenini. Kibarua kinachofuata ni dhidi ya Al Ahly mabingwa watetezi, Uwanja wa Mkapa.

    Nyumbani kwa moto

    Wakati Yanga wakianzia ugenini, moto uliwaka kwa wawakilishi Simba ambao Novemba 25 walikuwa mashuhuda ubao wa Uwanja wa Mkapa ukisoma Simba 1-1 ASEC Mimosas.

    Waligawaa pointi mojamoja na kutimiza mechi tano za kimataifa bila kuambulia ushindi. Katika mechi hizo Simba ilicheza tatu Ligi ya Mabingwa Afrika na mbili African Football League kote ilikuwa mwendo wa saresare.

    Kocha mpya kwa Simba

    Ni mrithi wa mikoba ya Roberto Oliveira, Abdelhack Benchikha ameanza kuwapa mbinu wachezaji wa timu hiyo. Huenda kazi yake ya kwanza ikawa dhidi ya Jwaneng Galaxy ugenini katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika.

    Hasira kwa Mkapa

    Yanga wanarejea Bongo wakiwa na hasira kwa kupoteza mchezo wao. Ni kete ngumu kucheza dhidi ya mabingwa watetezi Al Ahly kwenye mchezo unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa.

    Simba pasua kichwa

    Wawakilishi Simba ni pasua kichwa kutokana na mwendelezo wa makosa yaleyale kwenye kila mchezo wanaocheza kimataifa. Ni rahisi Simba kufunga kama ilivyo wao kufungwa. Hivyo ni nusunusu wapo kuambulia ushindi.

    Benchi la ufundi linakazi kubwa kuyafanyia kazi makosa kuanzia mlinda mlango, mabeki, viungo na washambuliaji.

    Mameneja wa Idara hawa hapa

    Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Yanga, Ali Kamwe ameliambia Championi Jumamosi kuwa wanatambua kazi kubwa iliyopo kwenye kusaka matokeo katika mchezo huo.

    “Ni mchezo mgumu ambao utakuwa na ushindani mkubwa lakini uzuri ni kwamba kila mchezaji yupo tayari kwa ajili ya mchezo huo hivyo wapinzani wetu watakutana na muziki uliokamilika.

    “Tutakuwa nyumbani mbele ya mashabiki wetu hivyo ni muda ni sasa kuelekea kupata burudani kwenye mchezo wetu wa ligi ya mabingwa baada ya kupoteza mchezo wa kwanza. Yale yaliyopita tumesahau tunasonga mbele.

    “Malengo ilikuwa ni kufika hatua ya makundi hilo limetimia na sasa tunahitaji kuona kwamba tunavuka hatua hii mpaka hatua ya robo fainali,”

    Ahmed Ally Meneja wa Idara ya Habari na Mawasiliano Simba amesema walipo hapo ambaye atawatoa ni wao wenyewe kwa kupambana kupata matokeo mazuri ugenini.

    “Mchezo wa kwanza tulianza nyumbani bahati mbaya tulipoteza pointi mbili. Hii ni ngumu kwetu na tumeanza vibaya kwa kuwa hatukutarajia kuwa hivi. Hakuna namna ambacho tunapaswa kukifanya ni kupata matokeo kwenye mchezo wetu ujao ugenini.

    “Ili kufikia malego yetu ni lazima turejee kwenye hali ya kujiamini kwa kupata matokeo ugenini. Inawezekana na wachezaji wanatambua kwamba ushindani ni mkubwa hilo lipo wazi,” .

    Previous articleWANAOKIMBIZA KWA PASI ZA MWISHO BONGO
    Next articleUWANJA WA LITI WAFUNGIKWA