KAZI BADO IPO KWA MASTAA HAWA YANGA NA SIMBA KIMATAIFA

    KUNA mambo mengine ni magumu kuyafanya sio kama sikukuu ya kumbukizi ya kuletwa duniani, ukiwa na keki inafanyika. Haina maana haiwezekani inawezekana kwa kuamua kufanya kweli, hivyo tu basi.

    Mastaa wa Yanga na Simba kwenye mechi za ligi ya ndani wamekuwa wakifanya kweli, anga la kimataifa ushindani unakuwa tofauti hivyo ni lazima waamue kufanya kweli pia.

    Matokeo ya mechi za mwanzo hayakuwa rafiki kwa timu zote hivyo ni lazima wafanye kazi kwenye mechi zinazofuata.

    Ikumbukwe kwamba Novemba 24 Yanga ilipoteza kwa kufungwa mabao 3-0 dhidi ya CR Belouizdad ya Algeria wakiwa ugenini kisha Novemba 25 Simba ilikuwa na kibarua dhidi ya Asec Mimosas Uwanja wa Mkapa na ikaambulia pointi moja.

    Hapa tunakuletea baadhi ya nyota waliosumbua ndani ya Ligi Kuu Bara wakiwa na kazi kufanya ndani ya anga la kimataifa namna hii:-

    Maxi Nzengeli

    Maxi kwenye ligi akiwa kacheza mechi 9 ni dakika 668 kazikomba mazima chini ya Kocha Mkuu, Miguel Gamondi. Ni mabao saba kibindoni anayo na pasi mbili za mabao akiwa na wastani wa kuwa na hatari kila baada ya dakika 74.

    Aziz

     Mguu wake wa kushoto ni chaguo lake la kwanza kuwatesa makipa ndani ya ligi. Aziz KI kwenye mechi 8 kakomba dakika 612 na pasi moja ya bao akiwa na hatari kila baada ya dakika 76.

    Pacome

    Pacome Zouzoah kacheza mechi 7 kayeyusha dakika 570 ni mabao manne katupia na pasi moja ya bao.Ana hatari kila baada ya dakika  114.

    Clement Mzize

    Mzawa anayezidi kuwa imara chini ya Gamondi kahusika kwenye mabao manne ndani ya ligi. Ni pasi mbili za mabao katoa akiwa katupia bao moja kwenye mechi sita akikomba dakika 390.

    Djigui Diarra

    Chaguo la kwanza kwa Gamondi akiwa kaanza langoni kwenye mechi 6 kakomba dakika 540 kafungwa mabao matano akiwa hajafungwa kwenye mechi nne.

    Shomari Kapombe

    Beki wa Simba, Kapombe uzoefu wake na uwezo haufichiki akiwa katika ubora wake. Ndani ya ligi katoa pasi mbili za mabao.

    Moses Phiri

    Ni yeye mzee wa saluti uwezo wake upo kwenye mguu wa kulia akiwa katupia mabao matatu ndani ya ligi na pasi moja ya bao kwenye mchezo dhidi ya Namungo, Uwanja wa Uhuru.

    Jean Baleke

    Ni namba moja kwa mastaa wenye mabao mengi wenye mabao mengi ndani ya Simba. Ni mabao saba kibindoni kwenye ligi hivyo ana kazi ya kufanya kwenye mechi za kimataifa.

    Kibu Dennis

    Mkandaji aliyekuwa chaguo la kwanza la Roberto Oliveira kabla hajasitishiwa mkataba wake. Ni bao moja alifunga kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Yanga, Novemba 5 2023 na alipoumia mipango ikavurugika.

    Clatous Chama

    Kasi yake haijawa kwenye ubora ndani ya msimu wa 2023/24 kwa kuwa kagota kwenye pasi moja ya bao na mabao mawili kwa muda mrefu.

    Haina maana kwamba hana uwezo ni mpaka pale atakapoamua kucheza hubadili hali ya upepo ndani ya uwanja. Kazi ni moja kufanya kweli kwenye mechi za kimataifa.

    Previous articleKUMEKUCHA YANGA, VYUMA HIVI HAPA VINAKUJA
    Next articleUKUTA WA SIMBA KUSUKWA UPYA