TAIFA STARS MAUMIVU INATOSHA

INATOSHA kwa maumivu ambayo mashabiki wameyapata pamoja na wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars ambayo ilikuwa ikipambana kwenye Kombe la Mataifa ya Afrika, (AFCON).

Kwenye mechi tatu ilizocheza ilikuwa ni ngumu kupata tabasamu kutokana na mechi zote kutoapa ushindi hivyo Watanzania wapo kwenye huzuni ya kuona kwamba kwa mara nyingine tena tunakuwa ni wasindikzaji kwenye mashindano haya makubwa.

Kuondolewa kwenye hatua za makundi mara kwa mara inamaanisha kwamba kuna mambo yanatakiwa kufanyiwa kazi kuanzia kwa wachezaji pamoja na uwekezaji kuwa mkubwa kwa mipango ya baadaye.

Hatua moja inapofika mwisho haina maana kwamba ni mwisho wenyewe bali ni mwanzo wa yale yanayokuja ukizingatia kwamba kuna mashindano mengine mbele.

Hongereni wachezaji kwa namna ambavyo mlijituma kutimiza majukumu yenu kwa wakati licha ya matokeo kutokuwa rafiki ni sehemu ya mchezo na mpira una maajabu yake.

Kucheza na timu kubwa inamaana kwamba nanyi kuna hatua ambayo mnatakiwa muwe hapo na kwa kufanyia kazi makosa wakati ujao mtakuwa imara na kutoishia kwa mara nyingine hatua ya makundi.

Benchi la ufundi limefanya kazi kubwa kuona namna gani kila mchezaji anapata nafasi kuonyesha uwezo wake lakini kilichotokea hakiwezi kubadili matokeo ni hayohayo muda wote.

Wakati ujao ni muhimu kufanya maandalizi mazuri ili kuwapa furaha mashabiki na wachezaji kutimiza malengo ya kuondoka katika hatua ya makundi mpaka 16 bora hili sio jambo la haraka mipango lazima ianze sasa.