MKIA UMALIZWE, WACHEZAJI WANALIA NA MENGI

MACHOZI ya wachezaji uwanjani yafutwe kwa vitendo na sio maneno yale ya kuwapa moyo kwamba haya yatapita. Kwenye mechi nyingi wanazocheza wapo wale wanaoumia kutokana na matokeo wengine hawajali.

Ipo wazi kwamba katika dakika 90 za kutafuta matokeo yapo mengi ambayo yanatokea.Kikubwa ni viongozi kuangalia kipi kinachofanyika baada ya mchezo.

Mashuhuda kwenye mchezo wa Kariakoo Dabi ambao ulikuwa na ushindani mkubwa. Mwisho mshindi alijulikana huku baadhi ya wachezaji waliopoteza wakitokwa na machozi.

Wanasema ukiona mtu mzima analia ujue kuna jambo. Pengine unaweza ukadhani labda wachezaji walikuwa wanalia kutokana na matokeo mabaya kumbe yapo mengine nyuma ya pazia.

Kikubwa kinachotakiwa kila kitu kinachowahusu wachezaji kizingatiwe kisichukuliwe kirafiki. Kama ni madai ya malipo ya stahiki zao wapewe kwa wakati ili kuendelea kupambania timu.

Ikiwa ni mfumo wa ubabe kwenye uendeshaji wa timu inapaswa kufanyiwa kazi. Makosa yapo lakini machozi yanapaswa kusitishwa kwenye mechi zijazo kwa wachezaji pamoja na viongozi.

Ikiwa umekula ng’ombe mzima mkia unagoma kuumaliza basi hiyo hali haitazimisha machozi ambayo yanatoka kwa sasa. Muda ni sasa kumalizia mkia ambao unasumbua kwa muda mrefu.

Ushindani ni mkubwa kwenye ligi na kila mmoja anahitaji kupata kile anachostahili baada ya dakika 90 ya mchezo. Kila la kheri kwenye mechi za ushindani kitaifa na kimataifa.