WAMOROCCO WANAWASHANGAA WACHEZAJI WA TANZANIA

    WACHEZAJI wengi waliopo Tanzania wamekuwa na kiwango kikubwa cha uchezaji lakini hawakuwahi kupitia katika shule za soka maarufu kama Academy.

    Ili mtoto awe bora ni lazima aanze kulelewa tokea akiwa mdogo akipata mafunzo ya mchezo husika ambao yeye anataka kuutumikia hapo baadaye.

    Watoto wengi wa Ulaya wamepata bahati kubwa ya kuwa na vyuo bora vya mafunzo na vimekuwa vikiwafanya wawe bora sana.

    Pamoja na hivyo, bado hata wenyewe wamekuwa wakipata wachezaji si kwa idadi wanayokuwa wameingia katika vyuo hivyo, kwamba wahitimu ni wachache sana.

    Kwa Tanzania vyuo ni vichache na wachezaji wengi ambao wanajifunza mpira mitaani wamekuwa wakicheza soka hadi kwenye viwango vya juu sana.

    Hii imekuwa mara nyingi ikitokana na Watoto wenyewe, kuwa na nia ya dhati kutaka kufikia ndoto zao na pia kuyakubali mazingira yao kuwa ni wachezaji ambao wanaishi katika mazingira ambayo hawawezi kupata msaada wa vyuo vya mafunzo vyenye ubora.

    Hivi karibuni timu ya vijana ya taifa ya wanawake chini ya umri wa miaka 17, ilicheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Morocco ambao walisafiri hadi Dar es Salaam.

    Mechi ya kwanza kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam iliisha kwa Tanzania kushinda kwa mabao 2-1.

    Kukawa na mechi ya marudiiano, Morocco wakatangulia kwa bao 1-0 lakini baadaye Tanzania wakasawazisha na mwisho wakashinda tena kwa mabao 2-1.

    Wachezaji wengi wa Morocco walishangazwa, maana walijua kwa mafunzo bora, vyuo walivyopita kwao Morocco na timu wanazocheza Ufaransa na Hispania ambazo zina vifaa na walimu bora wangejikuta wanashinda mechi zote tena kwa idadi kubwa ya mabao. Lakini haikuwa hivyo.

    Kilichotokea ni wao kuhoji kuwa vijana hao wa Kitanzania wanacheza timu gani za Ulaya. Walipoambiwa hakuna hata mmoja anayecheza huko wakajaribu kuangalia wangapi wanatokea Simba Queens au Yanga Princess, nako wakakutana hakutana.

    Wakaambiwa hao ni vijana mbalimbali waliokusanywa kwa juhudi za Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), wakawekwa kambini na kuanza kuandaliwa na sasa ndio wanagawanywa katika timu mbalimbali ili kujiendeleza zaidi. Wakashangaa sana.

    Waliona ni jambo la ajabu kutokea na wakaona ni vipaji vya kiwango cha juu ambavyo vinakua haraka na uwezo uko juu sana.

    Hawa wanashangaa, lakini sisi wenyewe kama Watanzania hatuoni. Hakuna anayeziona na kuziamini juhudi za TFF lakini hata klabu zenyewe bado hazioni umuhimu wa kukuza vijana kuanzia kwa wasichana hadi wavulana.

    Hapa kuna jambo la kujifunza kuwa pamoja na kwamba hatuna vifaa lakini tuna vipaji vya hali ya juu sana ambavyo kama tutawekeza tunakwenda kuwa gumzo na tishio Afrika.

    Maana kama wachezaji wanaocheza timu kubwa za vijana Ulaya, wanafungwa mara mbili na vijana ambao wamelelewa kwenye kambo moja kwa muda mfupi. Maana yake tuna kitu.

    Jiulize kama klabu zetu zingekuwa na malezi hayo bora na baadaye vijana hao wakajumuika kwa malezi na mafunzo tena chini ya TFF ingekuwaje?

    Lazima tukubali kuwekeza, soka halitaki haraka katika kila kitu na tukubali. Hata mazao yanayozalisha chakula ambacho tunakitegemea, huhitaji muda wakati wa makuzi yake shambani.

    Tuwekeze katika vijana na Serikali nayo iwekeze pia katika makuzi ya vijana ili vijana wetu waendelea kufanya vema, kupata ajira lakini kulitangaza taifa letu.

    Mechi mbili za ushindi wa vijana wetu dhidi ya Morocco ilikuwa ni Tanzania imeshinda na si TFF. Sasa Serikali iko wapi kuwekeza kwa vijana? Si sahihi kusubiri vijana hadi washinde ndio tuwazawadie kwa ushindi wakati makuzi yao tunakuwa hatuna Habari yoyote.

    Previous articleAFCON IPO VIZURI, MAANDALIZI MUHIMU
    Next articleHIVI NDIVYO MZAMIRU ALIVYOFANYA MAADILIKO YA KANOUTE CAF