Home Sports AFCON IPO VIZURI, MAANDALIZI MUHIMU

AFCON IPO VIZURI, MAANDALIZI MUHIMU

UWEKEZAJI mkubwa ambao unafanyika kwenye soka la Tanzania unaonekana. Kila siku milango ya fursa inazidi kufunguka, hili ni jambo kubwa ambalo linapaswa kuwa endelevu.

Tumeona namna ambavyo nafasi ya dhahabu ya kuandaa AFCON 2023 ilitangazwa, nchi tatu za Afrika Mashariki kupewa jukumu hilo. Uganda, Kenya na Tanzania zina kazi ya kufanya kwa maandalizi.

Hii ina maana kwamba kuna namna soka letu linazidi kupiga hatua. Kuwa wenyeji ni fursa itakayoendeleza soka letu kukua. Ushirikiano wetu uwe na faida kwenye kila idara.

Kinachotakiwa kwa sasa ni maandalizi mazuri. Kuanzia miundombinu na masuala ya uchumi ni muhimu kuwa tayari. Sio mbali ni karibu hivyo lazima kila kitu kiwe kwenye mpangilio mzuri.

Ukiachana na maandalizi kwa ajili ya AFCON bado kuna kazi kwenye soka la vijana. Huku ndiko ulipo msingi wa mandeleo ya soka letu kesho.

Ukweli ni kwamba ngazi ya vijana ni muhimu kutazamwa kwa ukaribu ili kuongeza nguvu kwa kuwa hawa wanatengenezwa kwa ajili ya kutumika kesho kitaifa na kimataifa.

Kukiwa na ongezeko la wachezaji kutoka timu za vijana wakiwa wanapewa nafasi pia kwenye timu za wakubwa taratibu watazidi kuwa imara kwa ajili ya mashindano makubwa.

Ili kuwa na wachezaji wengi wazawa ambao watafanya vizuri katika timu ya taifa ya Tanzania ni muhimu kuwa na sehemu nyingi za kuwatengeneza hasa kwenye timu za ndani.

Ikiwa ni timu chache zitakuwa zinawekeza nguvu kwenye kuwatengeneza wachezaji vijana hili litakuwa ni gumu kuwa na wazawa wenye uwezo mkubwa wakati ujao.

Kufanya vizuri kwa timu ya taifa ya Tanzania kunahitaji uwepo wa mwendelezo wa vijana ambao wanaandaliwa kwa wakati huu katika mashindano mbalimbali.

Vijana wana uwezo mkubwa wa kufundishika kuanzia kwenye timu walizopo. Wakipewa nafasi kwenye timu za wakubwa itaongeza hali ya kujiamini na kufanya vizuri zaidi.

Ni muda wa kuongeza nguvu pia kwenye uwekezaji katika soka la vijana kwenye kila timu hii itafanya wachezaji wengi wazalishwe kuanzia ngazi ya chini.

Uwekezaji ukiwa mkubwa unatoa fursa kwa timu kubwa kuwapa nafasi wale wachezaji kutoka ngazi ya vijana kucheza mechi za kimashindano jambo litakalowaongezea hali ya kujiamini.

Tukiwa na hazina ya vijana itaongeza uimara wa timu yetu ya taifa. Kuwa na timu bora kutaongeza hadhi ya ushindani kwenye anga la kimataifa.

 Wachezaji wazawa ni muda wa kuendelea kuwa tayari kwa wakati ujao. Kujituma na nidhamu ni muhimu kuelekea kwenye mafanikio. Ipo wazi kuwa hakuna mchezaji asiyependa kufikia malengo yake.

Kila timu ni wakati wake kuendelea kupambana kutengeneza wachezaji kwenye idara ya vijana nguvu ikiwa kubwa huku italeta matokeo mazuri.

Ikiwa hivyo hata kwenye mechi za kimataifa vijana wakiwa wanapewa nafasi watazidi kutambua namna hali ilivyo kwa kuwa ili uwe bora ni lazima ukutane na wapinzani bora kwa nyakati tofauti.

Kila kitu kinawezekana na muda bado upo kufanya maandalizi kwa ajili ya kesho bora kwa vijana waliopo nje na ndani ya timu.

Ukweli ni kwamba mchezo wa mpira ni mchezo wa wazi hauhitaji mambo mengi zaidi ya uwekezaji na kufanya kweli kwenye mechi za kitaifa na kimataifa.

Bado muda upo kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye uwekezaji wa vijana. Nguvu kubwa inapaswa kuwa endelevu kwenye eneo hili ambalo linahitaji usimamizi wa kweli.

Previous articleSINGIDA FOUNTAIN GATE KUJIPANGA UPYA
Next articleWAMOROCCO WANAWASHANGAA WACHEZAJI WA TANZANIA