SIMBA NA YANGA MAKUNDI WEKENI HESABU ZA LAZIMA

    SAFARI ya kwenda Rwanda, safari kwenda Zambia zote zilikuwa na upekee wake. Nianze na dua, Mwenyezi Mungu awatangulie ndugu zetu wafike salama na kurejea salama.

    Yanga ni Rwanda katika mechi yao ya kwanza  dhidi ya wageni wenzao El Merreikh ya Sudan ambao wamechagua kucheza Rwanda kutokana na matatizo ya vita nchini mwao.

    Wakati Simba wao safari yao ni Zambia, dhidi ya mabingwa wa nchi hiyo, Power Dynamo ambao tayari walifika hatua hiyo baada ya kufuzu katika hatua ya awali.

    Simba hawakucheza hatua ya awali kwa kuwa hapa nyumbani ilikuwa ni timu pekee iliyofanikiwa kusubiri katika hatua inayofuata wakati watani wao Yanga wakianzia katika hatua ya awali dhidi ya Asas ya Djibouti.

    Hii inakwenda kuwa mechi ya kwanza ya Simba ya kimataifa ya kimashindano na wanakwenda kuanzia ugenini. Hakuna ubishi ni lazima wawe wamejipanga kwelikweli.

    Kujipaga kwa maana ya kutengeneza wepesi katika mechi ya jijini Dar es Salaam kwa kuwa unapokuwa na matokeo mazuri katika mechi ya ugenini, basi unatengeneza nafasi ya kufanya kwa ubora zaidi katika mechi inayofuata.

    Advantage ni Simba kuanzia ugenini, hii inatoa nafasi ya kurekenbisha makosa ambayo unakuwa umeyafanya katika mechi iliyopita lakini ukizubaa mechi ya kwanza inaweza kuamua matokeo mapema kabisa.

    Kuanzia ugenini ni advantage lakini usipokuwa makini inawezekana kusiwe na faida yoyote. Mfano mzuri wanao Simba, waliwahi kuanzia ugenini dhidi ya Kaizer Chiefs na mwisho wakapoteza kwa mabao 4-0 wakiwa nchini Afrika Kusini.

    Waliporejea Dar es Salaam, walifanikiwa kushinda kwa mabao 3-0 wakipoteza nafasi nyingi, mwisho wakawa wametolewa kwa mabao 3-4. Jambo ambalo wanapaswa kulifanyia kazi kwa upana wa juu kwa kuwa tayari walishapitia hali kama hiyo na wanapaswa kukumbuka.

    Kufuzu kwa maana ya Simba kusonga hatua ya makundi inatakiwa kuwa ni jambo la “Lazima”, yaani wachezaji na benchi la ufundi la Simba lakini hata viongozi wajiwekee kuwa ni suala la lazima.

    Kweli kabisa, mpira unadunda lakini ni muhimu sana Simba kuamini mechi hiyo ni muhimu sana na ndio itatengeneza njia sahihi ya matokeo mazuri baadaye jijini Dar es Salaam.

    Kwa upande wa Yanga, Merreikh kweli wako nyumbani lakini Yanga wanaweza kuwa nyumbani zaidi lakini ni muhimu zaidi kujua mechi haijaisha na haiwezi kuisha kwa maneno tu.

    Merreikh ni timu ambayo licha ya kwamba wanapitia wakati mgumu kutokana na masuala ya nchi yao ya Sudan lakini wana malengo ya kufika mbali na wanajua faida ya wao kufanya vizuri na wakaingia hatua ya makundi.

    Pia wanajua kuwa sehemu kubwa ya wao kufanya vizuri ni kufanya vizuri katika mechi ya kwanza ambayo watakuwa ‘nyumbani’ mjini Kigali. Sababu Dar es Salaam wanapaswa kushuka wakiwa tayari na matokeo mazuri yanayowarahishia kazi.

    Hivyo haiwezi kuwa mechi ya utani kwao na hili Yanga waliweke kichwani lakini wajue kusonga mbele ni “Lazima” na mechi yenye majibu ni hii ya Kigali ambayo itaupunguza mlima kwa kiasi kikubwa kabla ya mechi ya Dar es Salaam.

    Mashabiki wa Yanga na Simba wamesafiri Rwanda na Zambia. Kuondoka kwao kumekuwa na hadithi nyingi kuhusiana na mabasi na mabasi madogo lakini mwisho ni kwamba mashabiki wamesafiri kwenda kuweka nguvu kama mchezaji wa 12.

    Niwakumbushe na mashabiki wenyewe, kwa kuwa kusonga mbele hadi makundi ni “Lazima”, basi ni muhimu sana sana wakaweka nia ya kufanya vema.

    Lazima wao nyeshe faida ya shabiki namba 12 kwa kushangilia kweli, kuongeza nguvu kweli na kupambana hasa kufanya mambo yaende kwa kiwango kinachoonyesha kulikuwa na faida ya wao kusafiri zaidi ya kilomita 1200 kwenda kuziunga mkono timu zao.

    Kufanya vizuri kwa Yanga na Simba katika mechi hizo za ugenini, ni faida na fahari ya Tanzania.

    Previous articleSIMBA KUSEPA BONGO MAPEMA KUWAWAHI WAZAMBIA
    Next articleSHABIKI YANGA AKOMBA MKWANJA MREFU NA M-BET