HAALAND AKOMBA TUZO

STRAIKA wa Manchester City, Erling Haaland
Alhamisi aliendelea kula matunda ya kazi
yake nzuri ambayo aliifanya msimu uliopita
akiwa na kikosi hicho baada ya kufanikiwa
kubeba tuzo ya Mchezaji Bora wa Kiume wa
Uefa.

Haaland ambaye alifunga mabao 36 kwenye
Premier msimu uliopita alibeba tuzo hiyo
kwenye hafla ya upangaji wa makundi wa Ligi
ya Mabingwa Ulaya (Uefa) Alhamisi
akiwapiku Lionel Messi na nyota mwenzake wa
Man City, Kevin De Bruyne.

Wakati straika huyo akibeba tuzo hiyo kocha
wake, Pep Guardiola yeye alifanikiwa kubeba
tuzo ya Kocha Bora wa Mwaka wa Uefa baada
ya kuisaidia klabu hiyo kubeba taji la Uefa
msimu uliopita wakiwafunga Inter Milan kwa
bao 1-0 kwenye mechi za fainali.