TFF YATOA UFAFANUZI KUHUSU WAZIRI WA MICHEZO NDUMBARO

SHIRIKISHO la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), limetoa taarifa kuhusiana na taarifa zinazoenea kwenye mitandao ya kijamii kuwa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dk. Damas Ndumbaro alifungiwa na shirikisho hilo kujihusisha na masuala ya michezo.

Taarifa iliyotolewa na TFF kupitia kwa Afisa Habari na Mawasiliano, Cliford Ndimbo, imeeleza kuwa Ndumbaro alifungiwa kutojihusisha na masuala ya michezo kwa miaka saba na uongozi uliopita wa TFF lakini alikata rufaa kupinga adhabu hiyo.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa Ndumbaro alikata rufaa kupitia Kamati ya Rufani ya Nidhamu ya TFF kupinga adhabu hiyo mwaka huohuo, 2017 ambapo alishinda rufaa hiyo na kufunguliwa.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa kwa sasa Waziri Ndumbaro ni Mwenyekiti wa Kamati ya Rufani ya Leseni za Klabu ya TFF.

Taarifa hiyo imetolewa rasmi Septemba 2,2023.