Home International YANGA NA SIMBA KILA UPANDE UMETOA TAARIFA LAKINI BADO

YANGA NA SIMBA KILA UPANDE UMETOA TAARIFA LAKINI BADO

MECHI ya kwanza ya Ligi Kuu Bara kwa mabingwa watetezi Yanga wakilitetea kombe lao kwa mara ya tatu mfululizo, imekuwa gumzo kubwa.

Hadi timu zaidi ya saba zikicheza mechi mbili za ligi kwa msimu wa 2023/24, Yanga walikuwa hawajacheza mechi hata moja kutokana na majukumu ya kimataifa.

Baada ya hapo, Yanga waliingia mtamboni kuanza kazi ya kulitetea taji lao na wakatoa kipigo cha mabao 5-0 dhidi ya KMC ya jijini Dar es Salaam.

Wakati wakishinda kwa idadi hiyo ya mabao, Simba na Azam FC ndio walikuwa wamefanikiwa kushinda kwa idadi ya mabao manne kila mmoja katika mechi walizocheza.

Azam FC walishinda kwa mabao 4-0 katika mechi ambayo wachezaji wa Kitayose wakiwa pungufu ana baadaye mechi hiyo ikavunjika. Simba wakashinda kwa mabao 4-2 dhidi ya Mtibwa Sugar katika mechi ambayo hadi mapumziko ilikuwa ni idadi ya mabao 2-2.

Ushindi wa Yanga wa mabao 5-0, maana yake Yanga ndio timu iliyofunga mabao mengi zaidi ya timu nyingine lakini iliyoshinda idadi kubwa ya mabao bila ya kuruhusu hata bao moja.
Tunaweza kusema vyovyote, kuwa KMC ni dhaifu, au KMC hawakuwa makini lakini jibu pekee ambao linaweza kutangulia ni kwamba Yanga walijipanga kuanza ligi kwa kasi kubwa sana.

Ushindi wao wa mabao Matano, maana yake wako tayari kupambana. Wako tayari kuhakikisha wanalitetea taji lao na wako tayari kwa ajili ya msimu mpya ambao kama wakibeba kombe kwao itakuwa ni mara ya tatu mfululizo.

Hakuna ubishi kuwa kikosi cha Yanga kilicheza vizuri na unaona, licha ya kumaliza kipindi cha kwanza wakiwa mbele kwa bao 1-0, kipindi cha pili Yanga walifunga mabao manne.

Hii maana yake, Yanga hawakuridhika na walikwenda kujipanga katika dakika 45 za mwisho kuhakikisha wanaongeza idadi ya mabao na kujihakikishia ushindi.

Mabao yao Matano, yote yamefungwa na watu watano tofauti, hii maana yake wana wigo mpana wa wanaoweza kufunga tofauti na msimu uliopita kuwa walimtegemea Fistion Mayele ambaye alikuwa mfungaji wao bora mfululizo kwa misimu miwili.

Simba wamecheza mechi mbili, hiyo moja walishinda kwa mabao 4-2 dhidi ya Mtibwa Sugar lakini wakashinda kwa mabao 2-0 dhidi ya Dodoma Jiji kwenye Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam katika mechi ambayo walipoteza nafasi nyingi za kufunga mabao.

Hali kadhalika, Azam FC licha ya kwamba walikutana na timu ambayo haikuwa imara kutokana na upungufu wa watu lakini bado walionyesha wana uwezo wa kufunga mabao zaidi pale inapotokea wakaipata nafasi.

Kumbuka kwa miaka kenda tisini, Simba, Yanga, Azam FC ndio wamekuwa vinara wa nafasi ya kwanza hadi ya tatu na wote wameonyesha wako tayari kwa ajili ya msimu mpya.

Hizi ni taarifa au salamu wanatupatia, kwamba wamejiandaa na wako tayari kwa ajili ya msimu mpya na wako tayari kwa ajili ya mapambano.

Hapa pia tunapaswa kuwakumbusha mashabiki ambao huenda wakawa wanaamini kuwa baada ya Yanga kushinda kwa idadi ya mabao Matano, basi atakuwa ameutetea ubingwa wake.

Tunapaswa kuwa na Subira kwa kuwa ligi ni ndefu na mambo yanakwenda yanabadilika, kuna timu ambazo zitakuwa zimeanza vibaya lakini baadaye zitabadilika na kusimama tena kwa kutengeneza picha tofauti na waliyoanza nayo.

Kuna timu ambazo zimeanza vizuri kama hawa vigogo, bado wanatakiwa kushikilia hapo na si jambo jepesi hata kidogo kwa kuwa ushindani unaendelea kuimarika.

Haina maana aliyeanza ligi kwa kushinda ma bao matano, basi kazi imeisha. Haina maana ushindi huo utamfanya asishishike kila mechi, haona maana kila atakayekutana naye atamfunga idadi hiyo.

Ndio maana nasema kuwa, wameanza vizuri na ujumbe wametutumia lakini bado tunahitaji kuvuta subira na kuendelea kuinjoy mchezo wa mpira kwa kuangalia nini kinafuatia.

Previous articleNMB YADHAMINI MASHINDANO YA GOFU
Next articleKOCHA YANGA ANAFIKIRIA MAKUBWA KUTOKA KWA KONKONI