ZIMETUPIA MABAO MENGI BONGO

    MTIFUANO mkubwa kwa wachezaji kusaka pointi tatu ndani ya uwanja unabebwa na kasi ya kuzitungua nyavu za walinda mlango ndani ya uwanja.

    Suala la kufunga ni muhimu ambapo kwa msimu wa 2022/23 mabingwa wa ligi ni Yanga.

    Kila timu ina mbinu zake kwenye kusaka ushindi na kuamua matokeo jambo linalofanya kila kitu kuwa kama ambavyo kimepangwa.

    Kwenye mwendo wa data tunakuletea timu saba ambazo zimefunga mabao mengi ndani ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2022/23 namna hii:-

    Simba

    Timu namba moja kwenye upande wa utupiaji mabao ni Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Robert Oliveira ikiwa imetupia mabao 66.

    Ni Moses Phiri huyu ni namba moja kwa utupiaji akiwa ametupia mabao 10 kibindoni na ametoa pasi tatu za mabao.

    Ikumbukwe kwamba kinara wa kutengeneza pasi ndani ya ligi yupo ndani ya Simba anaitwa Clatous Chama ametoa jumla ya pasi 14 na ametupia mabao manne.

    Moja kati ya pasi hizo alitoa kwenye mchezo dhidi ya Yanga.

    Yanga

    Yanga ni namba mbili kwenye timu zilizotupia mabao mengi ndani ya ligi ikiwa imetupia mabao 56 na inaongoza ligi ikiwa na pointi 74.

    Imetwa ubingwa wa ligi na ina mechi mbili mkononi huku kinara wa utupiaji mabao akiwa ni Fiston Mayele mwenye mabao 16 na ametoa pasi mbili za mabao ndani ya Yanga.

    Azam FC

    Ni Azam FC ya matajiri wa Dar hawa ni namba tatu kwenye safu zenye mabao mengi ikiwa imetupia mabao 45.

    Kinara wa utupiaji ni Idris Mbombo akiwa ametupia kibindoni jumla ya mabao 7 kimiani kwenye mechi za ligi.

    Geita Gold

    Namba nne ni Geita Gold  ikiwa imetupia mabao 33 ipo nafasi ya sita na kibindoni ina pointi 37 baada ya kucheza mechi 28 inanolewa na mzawa Felix Minziro.

    Singida Big Stars

    Namba tano ni Singida Big Stars ikiwa imetupia mabao 32 baada ya kucheza mechi 28 ndani ya ligi na kinara wa utupiaji ni Bruno Gomes ambaye ametupia mabao 9 kibindoni.

    Singida Big Stars kwenye msimamo ipo nafasi ya nne ikiwa na pointi 51 inanolewa na Hans Pluijm.

    Mbeya City

    Ikiwa nafasi ya 12 Mbeya City imekusanya pointi 30 imetupia mabao 31 kibindoni.

    Kinara wa utupiaji ndani ya Mbeya City ni Sixtus Sabilo ambaye ametupia jumla ya mabao tisa kibindoni ametoa pasi saba za mabao pia.

    Namungo, Tanzania Prisons na Mtibwa Sugar

    Timu hizi tatu zote kila moja imetupia mabao 28 zikiwa na wastani wa kufunga bao moja kila mchezo mmoja ndani ya msimu wa 2022/23.

    Namungo kwenye msimamo ipo nafasi ya tano ikiwa na pointi 39, Tanzania Prisons ipo nafasi ya 8 ina pointi 34 huku Mtibwa Sugar ikiwa nafasi ya 14 na pointi zake ni 29 kibindoni.

    Previous articleHIZI HAPA ZITAKUWA KWENYE KIVUMBI LEO
    Next articleMTAMBO WA MABAO WAPIKWA UPYA SIMBA