Home International EL CLASICO NI CLASSIC

EL CLASICO NI CLASSIC

LEO Alhamisi kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu wenye uwezo wa kuingiza mashabiki 81,044 kutakuwa na mechi kali ya wapinzani wa jadi nchini Hispania, kati ya Real Madrid na Barcelona, maarufu kama El Clasico.

Ndiyo, El Clasico maana yake ni ‘The Classic’, ikimaanisha mechi kati ya Madrid na Barcelona ni bora. Hii ni mechi ya watani wa jadi wa Hispania japokuwa wanatoka katika miji tofauti. Mchezo huo wa nusu fainali ya kwanza ya Copa del Rey unatarajiwa kupigwa saa 5:00 usiku kwa saa za Bongo.

Katika historia, mechi ya kwanza ya El Clasico ilichezwa mwaka 1902.  Mechi hiyo ilichezwa kwenye uwanja wa nyumbani wa Real Madrid, Santiago Bernabeu ikiwa ni ya michuano ambapo Barcelona ilishinda mabao 3-1.

Baada ya mechi hiyo zilichezwa mechi nyingi za kirafiki za El Clasico lakini katika historia ya La Liga, mechi ya kwanza ya El Clasico katika ligi hiyo ilichezwa Agosti 17, 1929 nyumbani kwa Barcelona, Camp Nou.

Real Madrid walishinda mechi hiyo kwa mabao 2-1 na kuwa ushindi wake wa kwanza katika El Clasico kwenye La Liga. Hadi leo katika La Liga zimechezwa mechi 185 za El Clasico tangu mwaka 1929, Real Madrid imeshinda mara 77, Barcelona imepata ushindi mara 73 na timu hizo zimetoka sare mara 35.

BARCELONA WABABE COPA DEL REY

Kwa mujibu wa takwimu za michuano ya Copa del Rey, Barcelona wameonekana kuwa wababe zaidi pande hizi kwani walipokutana na Madrid waliwafunga mara 15 huku Madrid wakishinda mara 12 huku wakitokea sare 8.

Ndani ya mechi hizo 35, imeshuhudiwa Barcelona wakiwa mwiba zaidi kwenye utupiaji ambapo wamefunga mabao 67 dhidi ya 65 ya Madrid.

MATAJI NA VIPIGO VIKUBWA

Barcelona ndio timu inayoongoza kwa mataji mengi ya michuano hii ya Copa del Rey wakibeba 31 na Madrid wanayo 19 tu.

Ndani ya uwanja kwa watani hawa imeshuhudiwa Madrid ikishikilia rekodi ya kutoa kipigo kikubwa zaidi kwa Barcelona cha mabao 11-1 hiyo ilikuwa Juni 19, 1943 wakati Barcelona wao kipigo kikubwa zaidi walichotoa kilikuwa Barcelona 6–1 Real Madrid ilikuwa Mei 19, mwaka 1957.

VITA YA BABA NA MWANA

Unaweza kusema hii ni mechi ya baba na mtoto kutokana na bosi wa Madrid, Carlo Ancelotti wakato akiinoa klabu hiyo miaka ya nyuma kocha wa sasa wa Barcelona alikuwa bado anacheza lakini sasa ni kocha wa klabu hiyo.

Kabla ya mechi yao ya juzi Jumapili, Xavi Hernández, 43, alikuwa ameiongoza Barcelona katika michezo 35 ya michuano yote msimu huu, kati ya hiyo ameshinda 25 sare tano na kufungwa mitano. Ana asilimia 71.43 za ushindi sambamba na kufunga mabao 2.14 kwa mechi na anaruhusu kwa wastani wa 0.83.

Kwa upande wake babu Carlo mwenye miaka 63, ameiongoza Madrid katika mechi 36 kati ya hizo ameshinda 25, sare sita na kupoteza mitano. Ana asilimia 69.44 za ushindi huku kikosi chake kikiwa na uwezo wa kufunga mabao 2.17 kwa mechi na kuruhusu kwa wastani wa 0.92.

Hata hivyo, Kocha wa Madrid, Ancelotti kwa upande wake anaonekana kuwa na kibarua kigumu katika ulinzi kwani inaonekana safu yake inapitika na kuruhusu mabao mengi wavuni ndio maana wamefungwa mabao 18.

BENZEMA KUSAKA REKODI YA MESSI

Ukitazama rekodi za El Clasico bado zinambeba Lionel Messi aliyekuwa akikipiga Barcelona kwani kwa muda wote kikosini hapo ndiye kinara wa mabao kwenye michuano hii ya Copa akifunga mabao 18.

Lakini kwa wachezaji ambao wanacheza kwa sasa kwa timu hizo ni Karim Benzema ndiye mwenye mabao mengi akiwa nayo nane hivyo anahitaji mabao 10 kuifikia rekodi hiyo, pengine anaweza kufanya kitu kesho kwakuwa mpira unadunda.

Previous articleMASHABIKI MNASTAHILI PONGEZI,WACHEZAJI KAZI IPO
Next articleYANGA NGOMA MPAKA ROBO FAINALI CAF