Home International MSHINDI WA TATU KUSAKWA LEO KOMBE LA DUNIA

MSHINDI WA TATU KUSAKWA LEO KOMBE LA DUNIA

TIMU ya Taifa ya Morocco leo Jumamosi inatarajiwa kumenyana na Timu ya Taifa ya Croatia kwenye mchezo wa kusaka mshindi wa tatu Kombe la Dunia Qatar 2022.

Safari ya Croatia yenye Luka Modric kuwania taji la Kombe la Dunia iligotea mbele ya Timu ya Taifa ya Argentina yenye Lionel Messi hatua ya nusu fainali baada ya kupoteza kwa kufungwa mabao 3-0.

Croatia ilifika hatua ya nusu fainali baada ya kuifungashia virago Timu ya Taifa ya Brazil yenye Neymar Jr kwenye hatua ya robo fainali kwa ushindi wa penalti 4-2 ikiwa ni rekodi yao ya kutinga nusu fainali mara mbili mfululizo.

Mwaka 2018 Croatia waligotea nafasi ya pili mwaka huu walishinda mchezo mmoja pekee kwa muda wa kawaida kati ya mechi sita ambazo walicheza na walitoka suluhu kwenye mchezo wa ufunguzi dhidi ya Morocco na waliitungua Canada mabao 4-1 na mchezo wao wa mwisho hatua ya makundi ilikuwa 0-0 Ubelgiji.

Timu hiyo ilipita kwa penalti dhidi ya Japan na Brazil hivyo imekuwa na zali lake kwenye penalti katika Kombe la Dunia.

Morocco wao katika Kombe la Dunia waliziondoa timu tatu kati ya zile ambazo ziliorodheshwa kuwa miongoni mwa timu bora duniani ikiwa ni pamoja na Timu ya Taifa ya Ureno na jitihada zao ziligotea miguuni mwa Timu ya Taifa ya Ufaransa ambao ni mabingwa watetezi.

Ufaransa watakaocheza fainali Jumapili dhidi ya Timu ya Taifa ya Argentina walishinda mbele ya Morocco kwa mabao 2-0 hatua ya nusu fainali.

Ikumbukwe kwamba timu hizo zilipokutana mwaka huu kwenye hatua ya makundi kwenye Kombe la Dunia zilitoshana nguvu hivyo leo lazima mshindi apatikane kwenye mchezo utakaochezwa Uwanja wa Taifa wa Khalifa.

Previous articleBOSI SIMBA: MANZOKI NDIYO, BOBOSI HAPANA
Next articleUMAFIA MZITO, PHIRI, BOCCO WAACHIWA MSALA GEITA GOLD