Home Sports MSAKO WA POINTI TATU ZA YANGA MBELE YA POLISI TANZANIA

MSAKO WA POINTI TATU ZA YANGA MBELE YA POLISI TANZANIA

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Bara jana waliweza kuendelea pale walipoishia kwa kupata ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Polisi Tanzania kwenye mchezo wao wa kwanza wa ligi.

Wakiwa ugenini Uwanja wa Sheikh Amri Abeid waliweza kushuhudia bao moja la Polisi Tanzania likifungwa na Salum Kipemba ambaye alifunga bao hilo baada ya mpira wa nahodha wa Yanga Bakari Mwamnyeto aliyekuwa akiokoa hatari langoni mwake kumgonga kwenye Kipemba na kurudi alipokuwa Diarra Djigui.

Ilikuwa ni dk ya 34 bao hilo lilipachikwa kimiani na kuwafanya Yanga kuanza kasi ya kusaka bao na dk ya 41 Mayele aliweza kupachika bao la kusawazisha kwa Yanga.

Bao hilo lilitokana na pigo la faulo iliyopigwa na Djuma Shaban na kuwafanya mabeki wa Polisi Tanzania kuwa kwenye harakati za kuokoa na mpira ukakutana na Mayele ambaye aliujaza kimiani na kufungua akaunti ya mabao.

Mayele alifuta kosa lake la kukosa penalti dk ya 11 ambayo iliokolewa na kipa wa Polisi Tanzania, penalti hiyo ilisababishwa na beki wa Polisi Tanzania Juma Kukuti ambaye alimchezea faulo Jesus Moloko na kwa kosa hilo mwamuzi wa kati Ramadhan Kayoko alimuonyesha kadi ya njano.

Kiungo Aziz KI ambaye alianza kwenye mchezo wa jana ikiwa ni mchezo wa kwanza kwake kwenye ligi akijiunga na timu hiyo akitokea ASEC Mimosas alipewa jukumu la kupiga kona ilikuwa dk ya 17 na alipiga shuti moja lililolenga lango ilikuwa dk ya 2.

Kipindi cha pili Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi aliweza kufanya mabadiliko kwa kumuingiza mzee wa kuchetua Bernard Morrisons aliyechukua nafasi ya Dickson Ambundo na Feisal Salum aliingia kuchukua nafasi ya Gael Bigirimana ilikuwa dk ya 57.

Morrison aliweza kutoa pasi yake ya bao dk ya 85 ilikutana na Mwamnyeto ambaye aliweza kupachika bao hilo la ushindi.

Polisi Tanzania walikamilisha dk 90 wakiwa pungufu baada ya nahodha wa timu hiyo Mohamed Mmaga kuonyeshwa kadi nyekundu baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano kwenye mchezo huo ilikuwa dk ya 44 na 88.

Katika mchezo mwingine uliochezwa jana, Singida Big Stars iliweza kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Tanzania Prisons.

Previous articleKIUNGO SERGIO GOMEZ NI MALI YA CITY
Next articleMZUNGU WA SIMBA ABAINISHA ATAREJESHA FURAHA KWA MASHABIKI