UONGOZI wa Azam FC umeweka wazi kuwa mseleleko ambao waliopata kuinasa saini ya kiungo kutoka Coastal Union Abdul Hamis Suleiman,’Sopu’ umetokana na kuwa na marafiki ndani ya Azam FC ambao ni wachezaji pia.
Sopu alikuwa kwenye hesabu za Coastal Union wenyewe ambao walikuwa kwenye mazungumzo ya kumuongezea mkataba,Simba na Yanga nao wanatajwa kuwa walikuwa wanahitaji saini yake.
Azam FC tayari imeshamtambulisha Sopu na msimu ujao wa 2022/23 atakuwa na uzi wa Azam FC ambapo kwa sasa wanamuita Mr Hat Trick kwa kuwa aliwatungua Yanga kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho.
Ofisa Habari wa Azam FC,Zakaria Thabit amesema kuwa hakukuwa na ugumu kumpata kijana huyo kutokana na kuwa na sababu zilizomvuta ndani ya Azam FC.
“Tumepata saini ya kijana chipukizi kutoka Coastal Union ambaye ni maarufu kwa jina la Sopu,imekuwa rahisi kumpata kijana huyu kwa kuwa yeye ni mkazi wa Mbagala.
“Pia Pascal Msindo,Tepsi Evance hawa anacheza nao kwenye timu ya Taifa ya Tanzania ya vijana hivyo imekuwa rahisi kumpata kijana huyu kwa kuwa anapenda kuwa karibu na wachezaji wenzanke,” amesema Zakaria.
Sopu anakuwa ni mchezaji wa pili kutambulishwa Azam FC kwa wazawa ambapo mzawa wa kwanza alikuwa ni Cleophance Mkandala kutoka Dodoma Jiji.