Home Sports USAJILI WA KIUNGO MNIGERIA SIMBA KAMA MUVI

USAJILI WA KIUNGO MNIGERIA SIMBA KAMA MUVI

NI kama muvi! Ndivyo utakavyoweza kusema baada ya Simba kuwazidi ujanja Azam FC katika usajili wa kiungo mkabaji wa Coastal Union, Victor Akpan na kumpa mkataba wa miaka miwili.

Timu hizo mbili zilikuwa katika vita kubwa ya kuwania saini ya kiungo huyo raia wa Nigeria aliyekuwa anawaniwa vikali na Azam katika kuimarisha safu yao ya kiungo inayochezwa na Sospeter Bajana, Mudathiri Yahaya na Frank Domayo anayetajwa kuachwa mwishoni mwa msimu huu.

Ndani ya Simba, Akpan anakwenda kuchukua nafasi ya Mganda, Taddeo Lwanga ambaye anatarajiwa kuachwa mwishoni mwa msimu huu.

Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Spoti Xtra kutoka ndani ya Bodi ya Wakurugenzi, Simba imefanikisha usajili wa Akpan Alhamisi iliyopita saa tano usiku ikiwa saa chache mara baada ya mabosi ya Azam kutoka kuonana na mchezaji huyo wakiwa kambini katika hoteli moja iliyopo Magomeni, Dar.

Mtoa taarifa huyo alisema, Azam ndio walikuwa wa kwanza kufika kambini hapo saa mbili usiku na kufanya mazungumzo na kiungo huyo na kufikia makubaliano ya kusaini mkataba kesho yake Ijumaa kwa kumpa mkataba wa miaka miwili kwa dau la Sh 150Mil.

Alisema kuwa, mara baada ya mabosi wa Simba kupata taarifa hizo, haraka saa tano usiku walivamia katika kambi hiyo na kumchukua kiungo huyo kwa bodaboda na kwenda naye kwenye moja ya hoteli kubwa kumpa mkataba wa miaka miwili kwa dau la Sh 100Mil.

Aliongeza kuwa, kwa kipindi hicho chote kiungo huyo atalipwa mshahara wa Sh 6Mil huku akipewa nyumba nzuri ya kuishi.

“Akpan huenda akatambulishwa Simba kesho (leo) Jumanne mara baada ya viongozi kufanikiwa kushinda vita kubwa ya kuwania saini yake kati yetu na Azam ambao walikuwepo katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wake.

“Haikuwa vita ndogo kufanikisha usajili wa Akpan, kwani Azam wenyewe walionekana kuwa siriazi kumsajili, lakini umafia tuliotumia tukafanikisha usajili wake wa miaka miwili kwa dau la Sh 100Mil, kati ya fedha hizo, Sh 20Mil zimekwenda Coastal kuununua mkataba wake wa mwaka mmoja uliobaki.

“Azam ndio walikuwa wa kwanza kumfuata kambini walipofikia Dar, mara baada ya kupata taarifa za Azam kumfuata na kufanya naye mazungumzo, basi sisi haraka siku hiyohiyo tukavamia kambini hapo na kumchukua kwa bodaboda na kumpeleka moja ya hoteli kwa ajili ya kumsainisha,” alisema mtoa taarifa huyo.

Alipotafutwa Akpan kuzungumzia hilo alikiri kuwepo katika mazungumzo na timu hizo mbili kwa kusema: “Hivi karibuni itajulikana wapi nitakwenda, lakini ukweli ni kwamba nipo katika mazungumzo na timu hizo mbili za Simba na Azam.”

Previous articleTULIA AIPA TANO TASWA FC,M-BET WATOA NENO
Next articleKOCHA MPYA SIMBA ATUA NA MAJEMBE MATATU YA KAZI