Home Sports TULIA AIPA TANO TASWA FC,M-BET WATOA NENO

TULIA AIPA TANO TASWA FC,M-BET WATOA NENO

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Tulia Ackson ameipongeza timu ya Waandishi wa Habari za Michezo nchini (Taswa SC) na Bunge SC kwa kupromoti michezo kwa kuonyesha mfano kwa vitendo kwa kucheza katika mechi mbalimbali.

Spika Ackson amesema hayo wakati wa mechi maalum ya kirafiki kati ya Taswa SC na Bunge SC iliyofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma na Taswa SC kuibuka na ushindi wa mabao 2-0.

Amesema kuwa amevutiwa na jinsi Wabunge na Waandishi wa Habari na Wabunge wakionyesha vipaji vyao katika mpira wa miguu na netiboli, jambo ambalo litawafanya vijana kuiga mfano wao na kupata wachezaji nyota wa timu za Taifa.

“Kwa kweli hii imenivutia sana kwani tutawafanya vijana kuiga mfano na kuwa na wachezaji bora, nawatakia kila la kheri katika jambo hili,” amesema Ackson ambaye pia ni mmoja wa wachezaji nyota wa netiboli wa timu ya Bunge Queens.

Mbali ya Ackson, pia Mama Salma Kikwete ni mmoja wa wachezaji nyota wa timu ya Bunge Queens ambayo inajiandaa na michuano ya Bunge la Afrika Mashariki yaliyopangwa kufanyika Juba, Sudan Kusini.

Kwa upande wake, meneja masoko wa kampuni ya michezo ya kubahatisha ya M-Bet Tanzania, Allen Mushi amesema kuwa amefurahishwa na timu zote mbili na kampuni yao ipo tayari kusaidia timu zote katika shughuli mbalimbali za michezo na kijamii.

“M-Bet Tanzania inajisikia faraja zaidi kushirikiana na Taswa SC katika kufanikisha ziara na tukio hili, pia tupo tayari kusaidia timu ya Bunge SC katika masuala mbalimbali,” amesema Mushi.

Naye Mwenyekiti wa Taswa SC, Majuto Omary aliipongeza timu ya Bunge SC na kampuni ya M-Bet Tanzania kwa kufanikisha lengo lao la kucheza na waheshimiwa Wabunge kwa mara ya pili.

Nahodha wa timu ya Bunge SC, Cosato Chumi amesema kuwa wamepata kipimo kizuri kuelekea michuano ya Afrika Mashariki na kuipongeza Taswa SC kwa mchezo mzuri.

Wakati huo huo, Taswa SC iliendeleza rekodi yake ya kutofungwa mwaka huu baada ya kuifunga Bunge SC mabao 2-0. Mabao ya Taswa SC yalifungwa na Waziri Idd na Zicco George.

Katika mchezo huo, Taswa SC iliongozwa na Mwenyekiti wake, Majuto Omary huku Bunge SC ikiongozwa na kapteni fundi Cosato Chumi.

Mbali ya Majuto aka Ronaldo wachezaji wengine waliongara katika mechi hiyo ni Wilbert Molandi (nahodha), Edward Mbaga, Salum Jaba, Saidi Seif, Muhidin Sufiani, Hassan Habani na kipa nyota Ismail Shaaban.

Katika mchezo wa pili, Taswa SC iliifunga Utumishi Veterans mabao 3-0. Mabao ya Taswa SC yalifungwa na Waziri, Zicco na Mlanzi.

Katika netiboli, Bunge Queens iliendelea ‘kuinyanyasa’ Taswa Queens baada ya kuichapa kwa mabao 15-13.

Previous articleBANGALA, DJUMA KUPEWA MIKATABA MIPYA YANGA
Next articleUSAJILI WA KIUNGO MNIGERIA SIMBA KAMA MUVI