IMEELEZWA kuwa mshambuliaji namba moja ndani ya kikosi cha Yanga, Fiston Mayele alikuwa kwenye hesabu za mabingwa watetezi Simba.
Nyota huyo ni ingizo jipya ndani ya kikosi cha Yanga na amekuwa kwenye mwendo mzuri wa kucheka na nyavu huku akikubalika na mashabiki wengi ikiwa ni pamoja na wale wa Simba.
Mtindo wake wa kutetema umekuwa ni gumzo kila kona ambapo hivi karibuni shabiki wa Simba maarufu kwa jina la Mama Bocco alipokuwa akihojiwa na JembeSports aliweka wazi kwamba anaskia kuhusu Mayele.
“Naskia kwamba kuna mchezaji mmoja anaitwa Mayele huyu huwa anatetema na ninahofia kweli mechi yetu ijayo kama atatufunga ninajiandaa kuzimia,” amesema.
Habari zinaeleza kuwa kabla ya Mayele kusaini Yanga, mabosi wa Simba walikuwa kwenye mpango wa kuinasa saini yake.
“Mabosi wa Simba walikuwa wanahitaji saini ya Mayele lakini ilikuwa ngumu kuipata kwa kuwa Yanga wao tayari walikuwa wamekamilisha kila kitu.
“Kumpata kwa sasa itakuwa ngumu kwani anapata kila kitu ndani ya Yanga hivyo watani wa jadi wanapaswa kujipanga kwa kweli wafanye mambo mengine ila sio saini ya Mayele mwenye mabao 11 kwenye ligi,”.
Mwenyekiti wa Simba, Murtaza Mangungu amesema kuwa kwa sasa sio wakati wa usajili hivyo nguvu kubwa ni kuelekea kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Orlando Pirates unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa, Aprili 17.