Home International MSOTO WA SIMBA KUSAKA POINTI MOJA KIMATAIFA ULIKUWA HIVI

MSOTO WA SIMBA KUSAKA POINTI MOJA KIMATAIFA ULIKUWA HIVI

JUU ni baridi kali hivyo jambo la muhimu ni kuweza kuongeza juhudi kupata nguvu zaidi zitakazorejesha lile joto asilia na njia ni moja tu kuendelea kushinda mechi zote ili kuongeza nguvu.

Wawakilishi wa Tanzania katika Kombe la Shirikisho Simba wakiwa katika hatua ya makundi na ni kundi D kwa sasa wanaongoza na pointi zao 4 baada ya kucheza mechi mbili za kimataifa.

Mchezo uliopita Uwanja wa General Seyni Kountche ulipigwa mpira wa kazi  na mwisho Simba iliambulia pointi moja  baada ya ubao kusoma USGN 1-1 Simba.

Hapa ni kumbukizi ya namna msako wa pointi moja ulivyokuwa chini ya Kocha Mkuu, Pablo Franco:-

Kosa moja bao moja

Ndani ya dakika 15 za mwanzo Simba walifanya kosa moja kupitia kwa wachezaji wake eneo la ulinzi likawagharimu wakatunguliwa na Wilfed Gbeulli dk 11.
Alikuwa ni Mohamed Hussein ambaye mpira wake wa kuokoa akiwa eneo la hatari ulipaa juu na kukutaba na wapinzani wake  kisha Sadio Kanoute naye katika harakati za kusepa  na mpira akapoteza ukakutana na wapinzani kwa mara nyingine tena na kuwapa nafasi wapinzani kupata bao la kuongoza.

Kipindi cha pili ukuta wa Simba ulifanya kosa kwa mara nyingine tena dk ya 60 kwa kumpa nafasi Abri Nasri aliyekosa kumtungua Manula akiwa ndani ya 18 kwa kuwa shuti lake lilikwenda nje ya lango.

Adebayo aliwapa shida

Victor Adebayo nyota wa USGN aliwapa shida wachezaji wa Simba kutokana na uwezo wake wa kupiga pasi na mashuti ambayo yalikuwa na hatari kwa Simba.

Pia jukumu la mipira iliyokufa lilikuwa miguuni mwake na aliweza kupiga faulo 3 na kona 5 pia alipiga shuti moja ambalo lililenga lango.
Njano sasa tatizo

Wachezaji wa Simba wanakazi kubwa ya kuweza kuongeza nidhamu kwa kuwa kadi za njano zinazidi kuongezeka kila mechi, mchezo uliopita dhidi ya ASEC Mimosas ni Peter Banda alionyeshwa kadi ya njano mbele ya USGN ni Zimbwe na Kanoute walionyeshwa kadi ya njano.

Umaliziaji tiba inahitajika 

Nyota wa Simba uwezo wa kutengeneza nafasi upo ila umaliziaji unahitaji tiba, Pape Sakho mashambulizi yake yalikosa utulivu alipiga mashuti mawili hayakulenga lango dk 11 na 14.
Zimbwe dk 26 shuti lake lilikwenda nje ya lango, Peter Banda dk 3 alipiga shuti nje ya lango, Meddie dk 61 alipiga shuti nje ya lango pia John Bocco dk 90 alipiga shuti ambalo halikulenga lango.

Shikamoo Manula

Air Manula alikuwa akitimiza majukumu yake na alikuwa akitumia mikono na miguu kulinda lango lake liwe salama.

Ukiweka kando bao moja alilotunguliwa aliokoa michomo 14 dk ya 1,8,9,10,11,19,29,30,31,39,52,54,67 na 85.
Hivyo inaonekana katika safu ya ulinzi  mambo ni magumu kwa Simba jambo linaloruhusu mipira kufika kwa Manula.

 Morrison 

Alipoingia dakika ya 64 Bernard Morrison akichukua nafasi ya Yusuph Mhilu bado yale makeke yake hayakuonekana mpaka zilipoyeyuka dakika 16 akaibukia katika kutupia bao dakika ya 83.

Pasi ya Shomari Kapombe ilitua katika kichwa cha Morrison ambaye hakuwa na namna zaidi ya kuuzamisha mpira wavuni.
Alitumia jumla dakika 26 sawa na Bocco ambaye alichukua nafasi ya Banda.

Majanga

Pascal Wawa beki kisiki aliingia dk 45 kuchukua nafasi ya Joash Onyango hakuyeyusha dk 45 alitoka dk ya 82 nafasi yake ikachukuliwa na Kened Juma.
Wawa alionekana kusumbuliwa na mguu jambo lililomfanya afanyiwe mabadiliko lakini kwa sasa yupo fiti.

Kituo kinachofuata 

Februari 27,2022 leo Jumapili itakuwa ni dhidi ya RS Berkane mchezo ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa mwanzo mwisho.

@dizo_click

Previous articleUWANJA WA MKAPA YANGA V KAGERA SUGAR VITA YA KISASI
Next articleMASTAA HAWA 6 WA YANGA KUIKOSA KAGERA SUGAR