KOCHA YANGA ANAFIKIRIA KUHUSU TAJI LA SIMBA

KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi amesema ushindi wa bao 1-0 walioupata dhidi ya Mbao FC kwenye Uwanja wa CCM Kirumba ni hatua nzuri kuwania Kombe la Shirikisho la Azam ambalo msimu uliopita walipoteza katika mchezo wa fainali.

Taji hilo lipo mikononi mwa Simba inayonolewa na Pablo Franco nayo imetinga hatua ya 16 bora kwa ushindi wa mabao 6-0 dhidi ya Dar City..

Yanga ilipata bao dakika ya 54 lililofungwa na Fiston Mayele akimalizia kwa kichwa mpira wa krosi iliyopigwa na Farid Musa.

Matokeo hayo yameifanya Yanga kufuzu hatua ya 16 ambapo sasa watakutana na Biashara United ambayo imetinga hatua hiyo baada ya kuiondoa Mbeya Kwanza.

  Nasreddine Nabi amesema ulikuwa mchezo mgumu kwani Mbao ni timu nzuri na kuwashukuru wachezaji kwa kupambana na kuibuka na ushindi.

“Ni jambo zuri kupata ushindi inakupa nguvu kuingia kwenye mchezo unaofuata ukiwa na ari na akili yetu tunaihamishia katika mchezo unaofuata ambao naamini hautakuwa rahisi,” alisema Nabi.

Kocha wa Mbao FC, Ibrahim Mumba alisema ubora wa Yanga hasa safu ya ulinzi  ulikuwa kikwazo kushindwa kutumia nafasi walizopata na kuwafanya kuibuka na ushindi kwenye mchezo huo.

 “Huu ulikuwa mchezo wetu muhimu kushinda katika mashindano ya Kombe la Shirikisho la Azam lakini tumeondolewa na sasa tunajipanga na michezo ya First League,” alisema Mumba.