>

KOCHA MPYA AZAM FC ASAINI MIAKA MITATU

OMAR Abdikarim Nasser amesaini dili la miaka mitatu kuwa Kocha Msaidizi mpya wa Klabu ya Azam FC inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Januari 29 alitambulishwa rasmi kuwa ni mali ya timu hiyo inayotumia Uwanja wa Azam Complex kwa mechi zao za nyumbani.

Kwa mujibu wa Azam FC wamebainisha kwamba ujio wake ni pendekezo la Kocha Mkuu wa Azam FC Abdihamid Moallin.

Nasser amewahi kufanya kazi katika nchi mbalimbali, mara ya mwisho 2019, akiitumikia moja ya vigogo vya nchini Qatar, Al Sadd, akiwa kama mchambuzi wa mechi (analyst) wa timu ya vijana chini ya umri wa miaka 23 (U-23).

Kabla ya kufanya majukumu kama hayo akiwa Al Duhail ya huko pia.

Al Sadd ni moja ya timu kubwa nchini humo, iliyokuwa ikinolewa na gwiji wa zamani wa Hispania, Xavi Hernandez, kabla kurejea Barcelona, akiwa kama Kocha Mkuu.

Omary, mzaliwa wa Somalia aliyekulia England na kuchukua uraia wa huko, pia alikuwa Kocha Msaidizi wa timu ya Taifa ya Somalia kuanzia mwaka jana hadi sasa.