KMC YACHEKELEA POINTI NNE UGENINI

UONGOZI wa KMC umeweka wazi kuwa pointi nne ambazo wamezipata ugenini zitawaongezea nguvu katika kurudi kwenye ubora wao.

Christina Mwagala, Ofisa Habari wa KMC amesema kuwa baada ya kukamilisha safari ya kusaka pointi sita na kupata nne ni hatua kubwa katika harakati za kurejea kwenye ubora.

“Tumetoka Dar tukaenda Sumbawanga, (Prisons 0-2 KMC) tukachukua pointi tatu na tulikuwa tunahitaji pointi tatu Mbeya, (Mbeya Kwanza 1-1 KMC) lakini tukapata pointi moja si haba ni makosa madogo ambayo yametufanya tukakosa pointi tatu.

“Fahari kwetu kurudi ugenini na pointi nne si jambo dogo ni jambo kubwa sana kwetu inaonesha kwamba hatupo mbali kwenye ule mkakati wetu wa kuweza kutoka hapa tulipo na kufika juu zaidi.

“Hii inatokea kwa sababu tunahitaji pointi tatu na tangu ligi inaanza hatukuwa na matokeo mazuri zaidi lakini inawapa morali wachezaji wetu kwamba tunahitaji kufanya vizuri zaidi hatupo nje kwenye mkakati wetu wa kuweza kufanya vizuri zaidi,” amesema Christina.

Kwenye msimamo KMC ipo nafasi ya 9 imekusanya pointi 15 huku Mbeya Kwanza ikiwa nafasi ya 12 na pointi zake ni 12 zote zimecheza mechi 13.