>

MASTAA YANGA WAPEWA ONYO NA NABI

KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, ameweka wazi kuwa hataki kuona nyota wake wakifanya makosa ya kupoteza nafasi yao ya kushinda ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu na kuwataka kuhakikisha wanacheza kila mchezo ulio mbele yao kama fainali.

Yanga ambao ni vinara wa msimamo wa Ligi Kuu Bara, hawakuwa na matokeo mazuri katika mashindano ya Kombe la Mapinduzi mwaka huu, kufuatia kuvuliwa kombe hilo katika hatua ya nusu fainali walipocheza dhidi ya Azam.

Jumapili Yanga iliweza kushinda mabao 2-0 dhidi ya Coastal Union kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara na kuwafanya wafikishe pointi 32 kibindoni.

Nabi amesema: “Tuliweka wazi tangu mwanzoni mwa msimu huu kuwa tunahitaji kushinda ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambao hatujashinda kwa kipindi cha miaka minne sasa, najua kuna namna wachezaji, viongozi na hata mashabiki hawajaridhishwa kuona tumepoteza Kombe la Mapinduzi.

“Lakini hatupaswi kusalia katika kuwazia hayo kwa kuwa tayari yamepita, jambo la muhimu ambalo nimewaambia wachezaji wangu ni kuwa lazima tuhakikishe tunauchukulia kila mchezo kwa uzito wake na kucheza kama fainali ikiwa tunahitaji kushinda ubingwa.”