KIUNGO wa Simba, Jonas Mkude, amefunguka kuwa kuchaguliwa kwake kuwa Mchezaji Bora wa Simba kwa mwezi Desemba, kumempa motisha ya kuendelea kupambana na kuendelea kuwa mchezaji muhimu ndani ya timu hiyo.
Mkude alisema tuzo hiyo ni kama deni kwa mashabiki ambao wamemchagua hivyo anatakiwa kuendelea kufanya kazi zaidi ili asiwaangushe wale ambao waliona kuwa alifanya kazi kubwa kuliko wengine mwezi uliopita.
Mkude aliibuka Mchezaji Bora wa Mashabiki wa Mwezi Desemba (Emirate Aluminium Simba ACP Fans Player of the Month),ambayo hutolewa kwa mchezaji chaguo la mashabiki.
Mkude amesema: “Hii tuzo imenipa hasira na hamasa ya kuendelea kupambana zaidi ili kuonyesha kuwa nilistahili kuwa mchezaji bora kwa mwezi husika. Nitafanya kazi zaidi na ikibidi niweze kuchukua tena hii tuzo.
“Wachezaji tuliofanya vizuri kwenye mwezi huo tulikuwa wengi, lakini wao wakaona mimi ndiye nimekuwa bora zaidi yao, ndiyo maana wakanichagua, sasa ni kufanya kazi tu.
Mchezaji wa kwanza kuchaguliwa kutwaa tuzo hiyo alikuwa ni Luis Miquissone msimu wa 2021/22 lakini kwa sasa maisha yake ya soka ni ndani ya Al Ahly ya Misri.