>

SAKHO ACHEKELEA KUTINGA FAINALI

PAPE Sakho, kiungo mshambuliaji ndani ya kikosi cha Simba amesema kuwa kwake ni furaha kuona timu hiyo inatinga hatua ya fainali ya Kombe la Mapinduzi.

Jana Januari 10, Sakho alikuwa ni miongoni mwa nyota walioanza kikosi cha kwanza mbele ya Namungo FC kwenye mchezo wa hatua ya nusu fainali ya pili.

Simba ilishinda mabao 2-0 na moja kati ya mabao hayo Sakho alifunga na bao lingine lilitupiwa na Meddie Kagere aliyanza kufunga dakika ya 14.

Baada ya mchezo kukamilika Sakho alipewa tuzo ya mchezaji bora wa mchezo na Shirika la Bima la NIC ilikuwa ni zawadi ya milioni moja.

Sakho amesema:”Furaha kubwa kuona kwamba tumeweza kutimiza lengo la kwanza la kutinga hatua ya fainali kisha baada ya hapo kazi itakuwa kwenye mchezo wa fainali.

“Jambo ambalo tunahitaji kuona ni furaha kwetu na mashabiki wa Simba, ushindani ni mkubwa na sisi pia tunafanya vizuri, mashabiki wazidi kuwa nasi,” amesema.

Kesho Simba itakuwa kwenye maandalizi ya mwisho kwa ajili ya  kibarua cha kusaka ushindi mbele ya Azam FC katika mchezo unaotarajiwa kuchezwa Januari 13.