REKODI zinaonyesha kwamba Azam FC wametwaa Kombe la Mapinduzi mara nyingi kuliko mpinzani wake Simba.
Hivyo Azam FC ni wababe mbele ya Simba kwenye Kombe la Mapinduzi kila wanapokutana kwenye mchezo wa fainali.
Azam FC imetwaa taji la Kombe la Mapinduzi mara tano huku Simba ikiwa imetwaa Kombe la Mapinduzi mara tatu.
Hii inakuwa ni mara ya nne Simba kuweza kukutana na Azam FC na kwenye fainali zote ambazo walikutana Azam FC iliibuka na ushindi na kusepa na Kombe la Mapinduzi.
Ilikuwa ni mwaka 2012,2017 na 2019 ambapo Azam FC walikuwa ni wababe kwa Simba hivyo Januari 13 itakuwa ni mara ya nne kuweza kukutana.
Januari 10 timu hizo mbili zilweza kutinga hatua ya fainali hivyo zinatarajiwa kukutana Alhamisi, Januari 13 kwenye mchezo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi.
Azam FC ilitinga hatua ya fainali kwa ushindi wa penalti 9-8 dhidi ya Yanga baada ya dakika 90 kukamilika kwa timu hizo bila kufungana na Simba ilitinga hatua ya fainali kwa ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Namungo FC.